Wateja TTCL wapunguziwa maumivu ununuzi Luku

Muktasari:

Akizungumza na waandishi wa habari jana, meneja mwendeshaji wa bidhaa wa shirika hilo, Nasra Muheiry alisema ofa hiyo imeanza jana na wateja wao watanunua Luku bila makato ya ziada.

 Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), limewaondolea wateja wake asilimia moja ya makato ya ziada wanaonunua umeme wa Luku katika kipindi cha miezi mitatu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, meneja mwendeshaji wa bidhaa wa shirika hilo, Nasra Muheiry alisema ofa hiyo imeanza jana na wateja wao watanunua Luku bila makato ya ziada.

Muheiry alisema kupitia mfumo wa TTCL Pesa na maduka ya huduma kwa wateja, wataweza kununua umeme wa Luku bila makato ya ziada.

“Madhumuni ni kuwarahisishia wateja na wananchi kwa ujumla kuweza kununua umeme wa Luku bila malipo ya ziada kwa unafuu zaidi kwa kutumia mtandao wa TTCL Pesa,” alisema Muheiry.

Naye meneja masoko wa TTCL, Aron Msonga alisema kabla ya ofa hiyo makato yalikuwa asilimia moja hivyo mteja atakayenunua Luku hatakatwa makato yoyote kwa miezi mitatu.

“Mfano, mteja wetu akinunua umeme wa Luku akitoa Sh10,000 atapewa uniti zake zote hatakatwa makato zaidi ya yale yaliyokuwapo awali,” alisema Msonga.

Alisema wateja waliojiunga na mtandao wa TTCL Pesa hadi sasa wamefikia idadi ya asilimia 30, hivyo ofa hiyo itasaidia watu kuongezeka na kwamba lengo lao ni kuongeza wateja zaidi waweze kutumia mtandao wa nyumbani.

Shirika hilo linalomikiwa na Serikali, lipo kwenye mikakati ya kujipanga upya baada ya kudorora kwa muda mrefu na tayari, limeshusha vifurushi vya inteneti ikiwa ni kuvutia wateja.