Watendaji kata 1,000 kuajiriwa

Muktasari:

  • Lengo ni kujaza nafasi zilizo wazi katika kata nyingi nchini

Dodoma. Serikali ina mpango wa kuajiri watendaji kata 1,000 ili kupunguza pengo kubwa la ukosefu wa watendaji hao katika maeneo mengi nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo bungeni na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Joseph Kandege.

Kandege alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Tundulu Kusini (CCM), Daim Mpakate ambaye alitaka kujua ni lini Serikali itaajiri watendaji kata kwani maeneo mengi yako wazi.

Naibu Waziri huyo alikiri watendaji ni watu muhimu katika shughuli za maendeleo hivyo Serikali imeona umuhimu wa kuwaajiri ili kusukuma mbele kurudumu la maendeleo.

"Tumeomba kibali na tumepewa kuajiri watendaji kata 1,000, hivyo tuna amini tukishaajiri hao tutakuwa tumepunguza pengo hilo kwa kiasi kikubwa," alisema Kandege.

Naibu Waziri huyo alisema mpango huo utafanyika mapema kwa kuwa uhitaji wao ni mkubwa.

Kuhusu posho za wenyeviti wa serikali za mitaa alisema kila halmashauri imekuwa ikisisitizwa kurudisha asilimia 20 ya mapato yake kwenye maeneo husika ili zisaidie kulipa posho za viongozi hao.