Haki za wasafiri kulindwa msimu wa sikukuu

Muktasari:

Chama cha kutetea abiria kimesema hakijapokea kesi ya utapeli au abiria kupandishiwa nauli.

Dar es Salaam. Chama cha kutetea abiria Ubungo, kimesema kuelekea msimu wa sikukuu za mwishoni mwa mwaka kimejipanga kulinda haki za wasafiri.

Imekuwa ni mazoea ifikapo mwishoni mwa mwaka, kituo cha mabasi yaendayo mikoani Ubungo (UBT) huwa na abiria wengi wanaosafiri kwa ajili ya sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

Kutokana na wingi wa abiria, baadhi ya wamiliki wa mabasi huongeza nauli; huku kukiwa na ulanguzi wa tiketi na utapeli.

Akizungumza na MCL Digital leo Jumatano Desemba 14,2017 mratibu wa idara ya barabara wa chama cha kutetea abiria (Chakua), Maulid Masaru amesema wamejipanga kukomesha utapeli, ulanguzi wa tiketi na kupandishwa nauli kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani.

"Maofisa wetu wanazunguka ndani na nje ya kituo kukagua na kuchunguza kama kuna utapeli unafanyika," amesema.

Amesema tangu Desemba Mosi,2017 hadi leo hawajapokea kesi ya utapeli au abiria kupandishiwa nauli.

Masaru amesema nauli haijapanda na abiria wanasafiri kwa nauli ya chini huenda ni kutokana na hali ngumu ya maisha.

Ofisa wa Sumatra ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kuwa si msemaji wa mamlaka hiyo aliyezungumza na MCL Digital, amesema hali ya usafiri si mbaya na hakuna abiria wanaoshindwa kusafiri.

Amesema wanatarajia wiki ijayo idadi ya abiria itaongezeka zaidi.