Watoto 11 milioni hatarini kufariki dunia kwa nimonia ifikapo 2030

Muktasari:

  • Ugonjwa hatari wa nimonia maarufu kama limonia umetajwa kuwa utaua watoto wengi zaidi katika muongo mmoja ujao.
  • Wataalamu watahadharisha nchi za ulimwengu wa tatu kuanza mapambano dhidi yake.

 

Dar es Salaam. Inakadiriwa kuwa takribani watoto 11 milioni wenye umri kati ya miaka mitano wanaweza kupoteza maisha kutokana na kasi ya ueneaji wa ugonjwa wa nimonia ‘Pneumonia’ ifikapo 2030, wataalamu wa afya wametahadharisha.

Ugonjwa huo unaonekana kusahaulika huku ukiwa tishio kubwa kwa nchi za ulimwengu wa tatu.

Tafiti zinaonyesha zaidi ya watoto 880,000 wenye umri chini ya miaka miwili walifariki kwa ugonjwa wa nimonia mwaka 2016 pekee.

Uchunguzi mpya uliofanywa na Chuo cha Johns Hopkins cha Marekani pamoja na Shirika la kusaidia Watoto la Save the Children, limebashiri kuwa kulingana na kasi ya ueneaji wa ugonjwa huo hivi karibuni, huenda ifikapo 2030 zaidi ya watoto  800,000 watashambuliwa na ugonjwa huo.

Ripoti hiyo imesema nchi ambazo zipo hatarini zaidi ni pamoja na Nigeria inayokadiriwa kufikia maambukizi ya Watoto 1.7 milioni, India (700,000) huku Pakistan ikikadiriwa kufikia maambukizi 635,000 .

Hatahivyo, wataalamu hao wanaeleza kuwa huenda ahueni ikapatikana endapo hatua za makusudi zitachukuliwa na kuweza kuokoa watoto 4.1 milioni ndani ya muongo mmoja ujao.

Ugonjwa wa nimonia au Pneumonia unaotokana na maambukizi kwenye mfumo wa hewa mwilini kwa njia ya bacteria, lakini unaweza kutibika kama utagundulika mapema.

Wataalamu wa afya wanasema ugonjwa huo unawashambulia zaidi watoto walioathiriwa na utapiamlo huku ukitajwa kuua zaidi kuliko malaria, kuhara na surua.

“Inasikitisha kuona karibu watoto milioni moja wanakufa kila mwaka kwa ugonjwa ambao tuna uelewa nao na tuna rasilimali za kupambana nao,” amesema Mkurugezi wa Shirika la Save the Children, Kevin Watkins.

“Hakuna uhamasishaji, mikutano ya kimataifa wala matembezi kwaajili ya kupinga ugonjwa huu, lakini kwa mtu yeyote anayejali haki za watoto katika kupata afya bora, ugonjwa huu uliosahaulika unatakiwa kupewa uzito mkubwa,” amesema mkurugenzi huyo.