Watoto wa Lucky Vincent kurejea nyumbani kesho

Balozi wa Tanzania nchini Marekani Wilson Masilingi akiwa na watoto Sadia, Doreen na Wilson pamoja na mama zao mjini Sioux City, Iowa nchini Marekani jana. Watoto hao ambao ni manusura wa ajali ya basi Shule ya Lucky Vincent ya jijini Arusha lililopoteza maisha ya wanafunzi 32, walimu wawili na pamoja na dereva wa basi hilo Mei 6 na kupelekwa nchini Marekani na Shirika la Samaritan Purse kwa matibabu wanatarajiwa kurudi nchini Ijumaa asubuhi kupitia Uwanja wa KIA . Picha na Mpiga Picha maalum

Muktasari:

  • Baba mzazi wa Doreen, Elibariki Mshana alisema anaamini mtoto wake atakuwa katika hali nzuri zaidi, lakini kwa namna anavyoona picha zake anazopata, anaona kwamba ingekuwa bora kama angeendelea kupata matibabu huko.

Arusha. Wanafunzi watatu wa Shule ya Msingi Lucky Vincent ya jijini hapa waliopelekwa Marekani kwa matibabu baada ya kuumia katika ajali iliyotokea Mei mwaka huu wanatarajiwa kurejea nchini kesho, lakini moja wa wazazi wao ameshauri wangeendelea kubaki huko kupewa matibabu.

Baba mzazi wa Doreen, Elibariki Mshana alisema anaamini mtoto wake atakuwa katika hali nzuri zaidi, lakini kwa namna anavyoona picha zake anazopata, anaona kwamba ingekuwa bora kama angeendelea kupata matibabu huko.

Doreen na wenzake wawili, Sadia Awadh na Wilson Tarimo, walinusurika katika ajali mbaya ya basi iliyosababisha vifo vya wanafunzi wenzao 32, walimu wawili na dereva mmoja iliyotokea Mei 6 katika eneo la Mlima Rhotia wilayani Karatu.

Mbunge wa Singida Kaskazini ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa taasisi ya Siouxland Tanzania Educational Ministries (Stemm), Lazaro Nyalandu alisema jana kuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuongoza mapokezi hayo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Wanafunzi hao walipelekwa Marekani Mei 14 kwa ajili ya matibabu yaliyoratibiwa Stemm kwa kushirikiana na shirika la ndege la Samaritan Purse linaloongozwa na Mchungaji Franklin Graham wa Marekani ukiwa ni msaada wa taasisi yake kwa Watanzania.

Wamekuwa wakipata matibabu katika mji wa Sioux, Jimbo la Iowa na baadaye Doreen alihamishiwa katika kituo cha Madona, kilichopo katika Jimbo la Nebraska kwa ajili ya mazoezi zaidi kutoka kwa wataalamu wa uti wa mgongo.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Nyalandu jana, ndege itakayowarudisha watoto hao ambao wameambatana na wazazi wao watatu, daktari bingwa Elias Mashala na muuguzi kutoka Hospitali ya Mount Meru, itawasili saa tatu asubuhi.

Mara baada ya kutua kwenye uwanjani wataelekea katika eneo maalumu lililotengwa kwa ajili ya familia za watoto hao pamoja wa wageni wachache kutoka katika Kijiji cha Mbuguni, Wilaya ya Arumeru (STEMM Village) ambako mjumbe wa Bunge la Congress la Marekani, Steve King na mke wake watahudhuria.

Nyalandu ambaye tangu watoto hao wakiwa Marekani amekuwa akituma taarifa za maendeleo yao kupitia mtandao wa Facebook, jana pia aliandika ujio wao kwenye ukurasa wake huo akiwaomba wananchi kujitokeza kuwapokea.