Watoto waenda mahakamani kutaka kujumuishwa

Muktasari:

Mke wa marehemu Mokiwa, Felister amesema baada ya mumewe kufariki dunia Septemba 12, 2014, kikao cha familia kilimteua kuwa msimamizi pekee wa mirathi.

Dodoma. Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita)  imezuia mali za aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa), marehemu Dk Peter Mokiwa kutokana na mgogoro wa mirathi kwa familia.

Mke wa marehemu Mokiwa, Felister amesema baada ya mumewe kufariki dunia Septemba 12, 2014, kikao cha familia kilimteua kuwa msimamizi pekee wa mirathi.

“Lakini hata kabla sijaanza taratibu za kufungua mirathi mahakamani, nilipata wito wa Mahakama nilipokwenda niliwakuta watoto wawili wa nje wa marehemu; Stella na Michael,” alisema.

Amesema hakimu alimhoji sababu za kukumbatia mali za baba yao bila kuwagawia  watoto, jambo ambalo lilimshangaza kwa sababu ilikuwa  muda mfupi tangu afiwe na mume.

Felister amesema licha ya kufikishwa mahakama ya wilaya, ilishindikana kugawana mali kwa sababu ya kuongezwa kwa msimamizi wa pili bila kupitishwa na kikao cha ukoo.

Amesema kushindwa kuelewana, Mahakama iliamua kuziweka mali hizo chini ya Rita tangu Machi mwaka huu huku akitakiwa kukabidhi nyaraka zote.

Shangazi wa Mokiwa, Catherine Kondokaya alisema  kikao cha ukoo kilimteua Felister kuwa msimamizi wa mirathi hiyo, lakini ghafla walisikia kuna msimamizi mwingine ameongezwa.

“Nilimfahamu Michael mwaka 2015 baada ya kujitokeza akidai ni mtoto wa marehemu, lakini hatukuwa na mawasiliano hadi tuliposikia ameongezwa kama msimamizi wa pili,” alisema.

Hata hivyo, Michael alipoulizwa kuhusu suala hilo, alikiri kumfahamu Felister kuwa msimamizi aliyeteuliwa kusimamia mirathi, lakini wao waliamua kupeleka barua mahakamani kuomba kuongezwa baada ya kuona hatekelezi majukumu yake.