Watoto wa familia moja waliokutwa wamekufa kwenye gari Dar wazikwa

Bibi wa watoto watatu wa familia moja waliokutwa wamefariki dunia kwenye gari, mtaa wa Njaro, Temeke, Dar es salaam, Amina Mohammed akisaidiwa kutoka nje ya nyumbani jana. Picha na Tumaini Msowoya

Muktasari:

Watoto watatu wa familia moja wamekutwa wamefariki dunia kwenye gari bovu aina ya Toyota Mark X baada ya kutoweka Oktoba 15, 2018 katika mtaa wa Njaro wilayani Temeke jijini Dar es Salaam

Dar es Salaam. Watu wa kada mbalimbali jana walijitokeza kuaga miili ya watoto watatu wa familia moja waliokutwa wamekufa wakiwa ndani ya gari baada ya kutoonekana kwa siku mbili.

Watoto hao waliokuwa wakiishi Mbagala jijini Dar es Salaam, walitoweka Oktoba 15 baada ya kwenda kumtembelea babu yao anayeishi Mtaa wa Njaro wilayani Temeke, na siku mbili baadaye walikutwa wamekufa kwenye gari aina ya Toyota Mark X.

Miili ya watoto hao, Mohammed (9), Amina Kunambi (7) na Yusuph Suleiman (2) ilifikishwa katika Msikiti wa Tungi, Temeke saa 9:45 alasiri na baadaye walizikwa katika makaburi ya Chang’ombe jijini Dar es Salaam.

Akisimulia tukio hilo, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Tungi, Amina Mlewa alisema alipata taarifa za kutoweka kwa watoto hao Oktoba 15 jioni.

“Tulipoambiwa watoto hawaonekani tuliwaambia watoe taarifa polisi kisha tukaanza kuwatafuta bila mafanikio,” alisema.

Alisema kwa kutumia kipaza sauti walipita katika mitaa mbalimbali wakitangaza kama kuna mtu aliyewaona lakini ilishindikana.

“Siku ya pili tuliambiwa kuna watoto wameonekana Mbagala, tulienda hadi huko bila mafanikio. Kweli nako kuna watoto walionekana lakini wazazi wao walikuwa wameshawachukua,” alisema Mlewa.

Alisema Jumanne iliyopita saa nne asubuhi walisikia kelele kutoka kwa babu yao na walipokwenda walikuta miili ya watoto hao katika gari.

“Nikalazimika kupiga simu polisi na zikaja gari mbili,” alisema mwenyekiti huyo akibainisha kuwa inavyoonekana watoto hao walijifungia katika gari hilo na kukosa hewa.

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Njaro, Abubakar Ahmed alisema gari walilokuwa wakicheza watoto hao mlango wake ulikuwa na uwezo wa kufunguka nje na sio ndani.

“Kwa hiyo walipoingia ndani ya gari na mlango kujibamiza hawakuweza kufungua tena,” alisema.

Ahmed alisema wakati watoto hao walipoaga kwenda kucheza, mwenzao mmoja aligoma kuondoka nao na kama angekubali wangekuwa wanne.

“Mungu mkubwa, huyu wa nne alikataa kuondoka na wenzake,” alisema. Alisema wakati wa kutoa miili hiyo ilibidi wabomoe kioo kimoja kutokana na gari milango kujifunga.

Waombolezaji washinda juani

Awali, miili ya watoto hao ilitakiwa kuwasili nyumbani kabla ya kuzikwa. Tangu asubuhi umati wa watu ulikuwa umefurika nyumbani kusubiri miili hiyo kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho.

Baadaye, Ahmed aliwatangazia kwamba miili hiyo haitafikishwa nyumbani kwa kuwa ilikuwa imeharibika.

Wataka uchunguzi

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walisema polisi wanatakiwa kufanya uchunguzi wa kina wa vifo vya watoto hao.

“Bado tuna maswali mengi sana kuhusu hawa watoto, ni kweli waliingia wenyewe au kuna aliwateka akaja kuwaleta baadaye? Bado hatuelewi inakuwaje mtoto wa miaka tisa akashindwa kufungua mlango wa gari,” alisema Athumani Hamis, mkazi wa Temeke.

Alisema katika siku tatu walizotumia kuwatafuta watoto hao wangeweza kugundua kama wapo ndani ya gari kwa sababu licha ya kuwa na kioo cheusi madirishani, kioo cha mbele kilionyesha ndani.

“Hata kama tunaambiwa walikufa kwa kukosa hewa lakini ichunguzwe tu kujua waliingiaje?” alihoji.