Watoto wanane wateketea kwa moto Kigoma

Muktasari:

Nyumba hiyo ilishika moto baada ya kutokea upepo mkali uliosababisha jiko la mafiga matatu linalotumia kuni lililokuwamo ndani, kukolea moto na kuunguza nyumba hiyo.

Kigoma. Watoto wanane wamefariki dunia baada ya nyumba waliyokuwamo kuungua moto katika kitongoji cha Tandala wilayani Uvinza.

Nyumba hiyo ilishika moto baada ya kutokea upepo mkali uliosababisha jiko la mafiga matatu linalotumia kuni lililokuwamo ndani, kukolea moto na kuunguza nyumba hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Fredinand Mtui alisema tukio hilo lilitokea juzi kwenye nyumba inayomilikiwa na Samke John, iliyojengwa kwa tofali na juu kuezekwa kwa nyasi.

Alisema kati ya watoto hao wawili ni wa mmiliki wa nyumba hiyo, watatu ni watoto wa dada mwenye nyumba, wengine watatu ni wa majirani zake.

Kamanda Mtui aliwataja majina ya watoto wa mwenye nyumba hiyo waliofariki dunia kuwa ni Masanja Samke (8) na Mjaliwa Samke (2), watoto wa dada yake ni Leonard Luhende (8) na Raphaeli Luhende (6) pamoja na Mariyam Bala, watoto wa majirani waliokutwa na mauti ni Hamiss Bala (6), Jala Magere (4) na Dutu Bala (2).

Alisema mwenye nyumba aliondoka nyumbani kwake takribani siku mbili zilizopita kwenda kufanya vibarua na kuwaacha wake zake wawili na watoto wao.

Kamanda Mtui alisema siku hiyo ya tukio saa sita usiku wake zake hao waliondoka kwenda kwenye sherehe ya ngoma za kienyeji, wakiwa pamoja na majirani na kuwaacha watoto wao wakiwa wamelala katika nyumba moja.

Alisema ilipofika saa saba usiku nyumba hiyo ilishika moto na kuteketea huku watoto hao wakiwamo ndani, jitihada za kuwaokoa zilifanyika lakini watoto watano walikutwa wamekwisha kufa papo hapo, watatu walifariki dunia katika kituo cha afya Nguruka.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga alisema Serikali itafanya uchunguzi ili kujua chanzo chake.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya, Nguruka Staphord Chamgeni alisema pamoja na jitihada za kuwanusuru watoto hao ilishindikana kutokana na majeraha waliyokuwa nayo.