Watoto zaidi ya miaka mitano wana nafasi kubwa ya kuishi nchini

Akizungumza katika mkutano wa 69 wa afya duniani uliofanyika Geneva nchini Uswisi, Mei 24, 2016 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache katika Bara la Afrika zilizofanikiwa kufikia lengo la nne la maendeleo ya milenia la kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano.

Muktasari:

  • 2,600: Watoto waliokadiriwa na Unicef kote duniani kufa ndani ya saa 24 za kwanza tangu kuzaliwa 2016. 
  • 9,400: Watoto njiti waliofariki dunia kutokana na huduma duni duniani mwaka 2015

  • 58%: Watoto waliozaliwa Mwaka Mpya kusini mwa Afrika wanatoka katika nchi tano, Tanzania ikiwamo. 

Dar es Salaam. Watoto wa sasa nchini Tanzania wana nafasi kubwa zaidi ya kuishi baada ya kuvuka umri wa miaka mitano kuliko wakati mwingine wowote, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) limesema.

Maniza Zaman, mwakilishi wa Unicef nchini, amesema utekelezaji wa programu za afya unaofanywa na Serikali umesaidia kuokoa maisha ya watoto.

Alisema wakati akitoa taarifa ya Unicef jana kuwa programu hizo ni kama vile utoaji wa mara kwa mara wa chanjo, nyongeza ya vitamini “A”, kuzuia maambukizo ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na kuimarisha udhibiti wa magonjwa yanayowaandama zaidi watoto.

“Lengo letu la pamoja ni kuimarisha jitihada na kumfikia kila mama na kila mtoto mchanga na kuwapa huduma bora ya afya,” alisema katika taarifa hiyo.

Alisema katika miongo miwili iliyopita, kumekuwapo na maendeleo makubwa duniani katika jitihada za kuokoa maisha ya mtoto, ambapo idadi ya vifo vya watoto kabla ya kutimiza umri wa miaka mitano imepungua kwa nusu hadi kufikia milioni 5.6 mwaka 2016.

Hata hivyo, alisema licha ya maendeleo hayo zipo changamoto kwa kuwa jitihada za upande wa watoto wachanga zimekuwa na mafanikio kidogo.

Unicef imesema takriban watoto 270 wenye umri chini ya miaka mitano hufa kila siku nchini Tanzania, na hasa kutokana na vyanzo vinavyoweza kuzuilika kama vile magonjwa ya malaria, mapafu na kuhara.

“Asilimia 60 ya vifo hivi hutokea ndani ya mwaka wa kwanza wa kuzaliwa. Kadhalika, mwezi wa kwanza wa kuzaliwa bado umeendelea kuwa na changamoto kubwa na asilimia 37.3 ya vifo vya watoto wachanga wenye umri chini ya miaka mitano hutokea ndani ya mwezi wa kwanza wa kuzaliwa,” inasema taarifa hiyo.

Katika mwaka 2016, vifo vya watoto wachanga katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara vilikuwa  asilimia 38 ya vifo vyote duniani.

Unicef ilisema Tanzania ni miongoni mwa nchi 10 duniani zenye viwango vya juu vya idadi kubwa ya vifo vya watoto wachanga.

Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa ya Level & Trends in Child Mortality 2017, watoto 136,000 wachanga walikufa na kati yao 90,000 ni wa nchini Ethiopia na 46,000 wa Tanzania, hivyo kuzifanya kushika nafasi ya tano na tisa miongoni mwa nchi 10 zenye viwango vya juu kabisa vya vifo vya watoto wachanga duniani.

“Zaidi ya asilimia 80 ya vifo vyote vya watoto wachanga, miongoni mwa watoto hao vilisababishwa na vyanzo vinavyozuilika na kutibika kama vile kuzaliwa njiti (kabla ya muda), matatizo wakati wa uzazi, maambukizi kama vile bakteria na homa ya mapafu,” inasema taarifa hiyo.

Katika mwaka 2016, Unicef inasema ilikadiriwa watoto 2,600 kote duniani walikufa ndani ya saa 24 za kwanza tangu kuzaliwa.

Takwimu zilizosomwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya wakati wa maadhimisho ya Siku ya Watoto Njiti duniani zinaonyesha katika mwaka 2015, kati ya watoto njiti zaidi ya 200,036 waliozaliwa, watoto 9,400 walifariki dunia kutokana na huduma duni.

Mkurugenzi wa Unicef wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Leila Pakkala anasema katika taarifa iliyotolewa na Unicef jana kuwa mkakati wa Unicef kwa mwaka 2018 ni kuhakikisha watoto wanapata nafasi ya kuishi kwa kutumia kampeni ya “Kila Mtoto Aishi” itakayozinduliwa Februari.

Kampeni hiyo aliyosema itafanyika duniani kote, itahimiza upatikanaji wa ufumbuzi wa matunzo ya gharama nafuu na bora ya afya kwa kila mama na mtoto mchanga.

“Ufumbuzi huu ni pamoja na upatikanaji wa uhakika wa maji safi na salama na umeme katika vituo vya afya, uwepo wa mhudumu wa afya mwenye mafunzo wakati wa kujifungua, kuzuia maambukizi katika kitovu, kunyonyesha mtoto ndani ya saa la kwanza baada ya kujifungua, mtoto kuwa karibu na mama kiasi cha kugusana, yaani mama kumkumbatia mtoto wake,” alisema.

“Tunaingia katika zama ambayo watoto wachanga wa sasa wana fursa ya kuja kuiona karne ya 22. Ni bahati mbaya kwamba karibu nusu ya watoto waliozaliwa mwaka huu hawatapata nafasi hiyo. Sisi sote tunaweza kufanya zaidi kuhusu hili,” alisema Leila.

Wakati huohuo, Unicef imebashiri kuwa takriban watoto 48,000 walitarajiwa kuzaliwa katika ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika katika siku ya Mwaka Mpya.

Unicef imeziomba nchi zote katika ukanda huo kuhakikisha watoto wengi zaidi wanaishi na kubaki salama katika siku ya kwanza maishani mwao.

Shirika hilo limesema watoto waliozaliwa mashariki na kusini mwa Afrika ni sawa na asilimia 12 ya watoto wachanga wanaokadiriwa kufika 386,000 waliozaliwa duniani katika siku ya Mwaka Mpya.

Alisema asilimia 58 ya vizazi hivyo ni katika nchi tano za ukanda huo, huku idadi ya juu zaidi ikiwa ni Ethiopia watoto 9,023, Tanzania (5,995), Uganda (4,953), Kenya (4,237) na Angola (3,417).