Thursday, September 14, 2017

Watu ‘wasiojulikana’ wauawa na polisi Ruvuma

 

By Joyce Joliga, Mwananchi

Songea. Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma limewaua watu wawili wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wakati wakirushiana risasi na polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Gemini Mushy amesema tukio hilo limetokea jana Jumatano saa 2:45 usiku katika Kijiji cha Nangungulu Wilaya ya Tunduru.

Alisema askari polisi wakiwa doria waliwaua wanaume wawili ambao wanakadiriwa kuwa na umri wa miaka 20-30 baada ya majibizano ya risasi.

Kamanda Gemini alifafanua zaidi kuwa watu hao walikuwa na silaha aina ya SAR na risasi zake 41 pamoja na pikipiki ambayo namba zake za usajili zimehifadhiwa.

Alisema polisi wakiwa doria waliona pikipiki ikiwa imesimama hivyo walisimama ili kuikagua ndipo abiria akitoa bunduki na kuanza kuwashambulia askari ambao nao walijibu mashambulizi na kufanikiwa kuwazidi maarifa na kupoteza maisha palepale.

Alisema katika tukio hilo hakuna askari aliyejeruhiwa wala kupoteza maisha.

Kamanda amewaomba wananchi kutoa taarifa za wahalifu  wanaojihusisha na matukio ya utumiaji silaha kama wanawafahamu au pindi wanapowatilia shaka.

Amewataka wananchi kujitokeza kutambua miili ya watu hao ili waweze kuchukuliwa na ndugu zao.

-->