Watu kuanza kujipima kifua kikuu kwa simu

Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile (wa tatu kulia) akizindua huduma ya uchunguzi binafsi wa ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) kupitia simu za mkononi jijini Dar es Salam jana. Picha na Omari Fungo

Muktasari:

Huduma hiyo yenye hatua muhimu 15 za dodoso za maswali, itamwezesha kila mwenye simu ya mkononi kuchunguza afya yake kwa kupiga *152*05# kisha kuchagua nambari sita.

Dar es Salaam. Wakati watu 74 hufariki dunia kila siku nchini kutokana na ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB), Serikali imezindua huduma za uchunguzi binafsi kuhusu ugonjwa huo kupitia simu za mkononi.

Huduma hiyo yenye hatua muhimu 15 za dodoso za maswali, itamwezesha kila mwenye simu ya mkononi kuchunguza afya yake kwa kupiga *152*05# kisha kuchagua nambari sita.

Baadhi ya maswali yanayohojiwa katika dodoso hiyo ni pamoja na umri wa mlengwa, eneo analoishi, jinsia na iwapo amewahi kuugua kikohozi kwa zaidi ya wiki mbili.

Akizindua huduma hiyo jana, Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema ugonjwa wa TB unaua watu 74 kila siku sawa na watu watatu kila saa moja.

Alisema Serikali imekuja na mkakati huo kwa lengo la kuwapata wale wanaoshindwa kuwafikia.

Alisema kwamba wizara itawezesha ufanisi na ufuatiliaji wa mfumo huo ili kuhakikisha taarifa zinakusanywa na kutumika ipasavyo.

“Tutaangalia idadi ya watu waliosajiliwa, idadi ya ujumbe uliotumwa kwa walengwa, idadi ya wagonjwa wa TB waliogundulika na ufuatiliaji wa wagonjwa kwa wakati muafaka. Matumaini yangu taarifa zitakazokusanywa zitakuwa muhimu kwa usimamizi wa mtu binafsi na program,” alisema Dk Ndugulile.

Alisema kupitia ujumbe wa uchunguzi binafsi, mtu yeyote anaweza kuingia na kujibu maswali kulingana na dalili za ugonjwa wa TB na baada ya kukamilisha iwapo mteja ana dalili za TB, mfumo huo utamwelekeza kwenda kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu, ataendelea kukumbushwa mpaka atakapokubali kwamba ametembelea kituo cha afya.

Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma, Dk Beatrice Mutayoba alisema huduma hiyo ni matokeo ya jitihada za dhati za mpango wa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya katika azma kuu ya kutokomeza kifua kikuu nchini ifikapo 2030.

Alisema matumizi hayo ya teknolojia itakuwa chachu muhimu katika kufikia malengo ya nchi katika uibuaji wa wagonjwa wanaokosa kugunduliwa kila mwaka na matokeo chanya kwa wagonjwa wanaotibiwa.

“Huduma hii inatambulika kama Tambua TB ambayo ni matumizi ya ujumbe mfupi wa simu za mkononi wenye nia ya kuongeza uelewa kuhusu Kifua Kikuu kwa jamii na kusaidia kuongeza kasi ya uibuaji wa wagonjwa pamoja na kuwahamasisha na kuwaelimisha wagonjwa walioko kwenye matibabu kuhusu ufuatiliaji mzuri wa matibabu,” alisema Mutayoba.

Meneja wa Mawasiliano wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando alisema kwamba walianza kutoa huduma za afya kupitia simu za mkononi kwenye kampeni ya ‘wazazi nipendeni’ na kufanikiwa kwa meseji milioni 31 kuingia.

Pia, aliongeza kwamba kinamama milioni tano wametibiwa magonjwa ya uzazi kupitia mfumo huo.

“Utaalamu na teknolojia zaidi, sisi watoa huduma tunazidi kujiimarisha ili kuhakikisha tunaisaidia jamii katika masuala ya afya,” alisema Mmbando.