Wajue watu mashuhuri waliowahi kutetewa na wakili Kibatala

Muktasari:

Tayari Kibatala ametua Mbeya kumwakilisha Mbilinyi maarufu Sugu.


Dar es Salaam. Peter Kibatala, ni wakili aliyejizolea umaarufu kutokana na kutetea watu maarufu na wenye kesi kubwa mbalimbali.

Miongoni mwa watu ambao wameshatetewa na wakili huyo ni msanii wa filamu nchini, Wema Sepetu aanayekabiliwa na  kesi ya matumizi ya dawa za kulevya iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, wakili huyo aliiandikia barua mahakama akiomba kujitoa kumwakilisha msanii huyo na siku hiyo hiyo mahakama hiyo ilipokea barua kutoka kwa wakili Albert Msando ambaye amemwakilisha leo Alhamisi Februari 8, 2018 akiomba kumwakilisha Wema.

Kesi nyingine ni ya naibu waziri wa zamani wa Fedha na Uchumi, Adam Malima ambaye kwa sasa ni mkuu wa Mkoa wa Mara aliyefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi ya  kushambulia.

Hata hivyo, kesi hiyo ilifutwa baada ya Malima kuteuliwa kuwa mkuu wa mkoa na mkurugenzi wa mashtaka (DPP) kueleza kuwa hakuwa na nia ya kuendelea nayo.

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ni miongoni mwa watu maarufu waliowahi kutetewa na wakili Kibatala katika kesi ya kushindwa kutunza silaha.

Pia, kesi hiyo ilifutwa baada ya upande wa mashtaka  kushindwa kuthibitisha mashtaka hayo na mahakama kuamuru arudishiwe mkoba wenye silaha yake.

Pia, mwanasheria mkuu wa Chadema na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu anatetewa na wakili Kibatala.

Wakili Kibatala ni miongoni mwa mawakili 18 wanaomtetea Lissu katika kesi ya kutoa kauli za uchochezi.

Mwingine ni msanii, Elizabeth Michael ‘Lulu’, aliyekuwa aliyeshtakiwa kwa kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Stephen Kanumba. Tayari, Lulu anatumikia kifungo cha miaka miwili jela baada ya Mahakama Kuu kumkuta na hatia Novemba 13, 2017.