Watu watano wafa mapokezi ya Raila yakikumbwa na vurugu

Wafuasi wa muungano wa Nasa nchini Kenya wakiandamana jijini Nairobi jana kumpokea kion-gozi wao Raila Odinga aliyerejea kutoka nchini Marekani. Picha na AFP

Nairobi, Kenya. Vurugu zilizoambatana na mabomu ya machozi na uchomaji matairi ni kati ya matukio yaliyogubika mapokezi ya kiongozi wa muungano wa Nasa, Raila Odinga katikati ya Jiji la Nairobi aliporejea jana akitokea Marekani alikofanya ziara ya siku 10.

Polisi walitumia mabomu ya machozi na maji ya kuwasha kuwatawanya wafuasi wa Nasa waliojitokeza kwa mamia kumpokea Raila.

Kuna madai kwamba risasi zilitumika na pia inadaiwa watu watano waliuawa katika vurugu hizo.

Gari la Raila lapigwa

Kioo cha mbele cha gari alilopanda Raila kiliharibiwa wakati polisi wakifukuzana na wafuasi wa kiongozi huyo. Hata hivyo, haikufahamika mara moja ikiwa kiliharibiwa kwa risasi au jiwe.

Kioo hicho kiliharibiwa katika Barabara ya Jogoo. Raila hakudhuriwa na msafara wake uliongoza moja kwa moja hadi Kibra ambako alihutubia mkutano mkubwa wa wafuasi wake.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Mwenda Njoka alitupilia mbali madai ya kuwapo jaribio la kutoa uhai wa Raila. “Madai kwamba lilikuwapo jaribio la kutoa uhai wa Raila ambayo yanasambazwa kwenye mitandao ya kijamii ni ya uongo na hayana msingi,” alisema katika ujumbe wa Twitter.

Njoka alisema madai hayo yanayosambazwa kupitia akaunti iliyothibitika kuwa ni ya muungano wa Nasa yana lengo la kuomba huruma. “Madai hayo yapuuzwe na yadharauliwe,” alisema.

Msafara wa Raila

Raila aliondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) katika msafara wa makumi ya magari yaliyoongozana na ya viongozi wa Nasa pamoja na mamia ya wafuasi wao.

Wafuasi wake walijimwaga mitaani tangu alipotua. Baadhi walilazimisha kufika na kuingia kwenye uwanja wa ndege ambako walizuiwa na polisi waliokuwa wamejihami kwa silaha, mabomu ya kutoa machozi, magari ya kurusha maji ya kuwasha na helikopta.

Baadaye hali ilibadilika kuwa ya vurugu na mapambano kati ya polisi na wafuasi wa Nasa ambao walikuwa wakichoma matairi barabarani, wakiweka vizuizi, wakiwakejeli polisi na kuwarushia mawe, vijinga vya moto huku wakiimba.

Vurugu zilianza baada ya msafara wa Raila kuondoka JKIA lakini ukaingia kimakosa katika barabara ya Mombasa. Hii ni kwa sababu barabara hiyo ilikuwa na msafara mrefu umbali wa kilomita kadhaa kutokana na mapambano ya polisi na wafuasi wa Raila.

Wafuasi wa Nasa walitaka kulazimisha kuingia kwenye uwanja wa ndege lakini polisi waliwarushia mabomu ya kutoa machozi eneo la City Cabanas na maeneo mengine ili kuwazuia.

Baadaye msafara huo uliacha barabara ya Mombasa na kuingia Barabara ya Jogoo lakini vurugu ziliufuata msafara wa Raila na wafuasi wake baada ya polisi kupambana na vijana waliokuwa wakirusha mawe.

Lengo lao lilikuwa kutembea kwa miguu katika Barabara ya Jogoo kisha Haile Sellasie halafu waende viwanja vya Uhuru Park, lakini ilishindikana kutokana na makabiliano ya ghasia.

Hasara

Mapambano kati ya polisi na wafuasi wa Nasa yalisababisha biashara kusimama katika barabara hiyo ya kibiashara upande wa mashariki mwa jiji.

Mzunguko katika Uwanja wa Jiji ulitulia baada ya polisi kuziba barabara katika juhudi za kuzuia vurugu kuenea katika maeneo mengine ya jiji. Kwa kipindi kirefu magari yalitulia huku vibanda vya biashara vikifungwa na wauzaji wakikimbia kwa usalama wao.

Basi dogo linalomilikiwa na kampuni ya Forward Travellers Sacco, lori la polisi na mikokoteni miwili vyote vilichomwa moto nje ya soko la Burma. Barabarani kulikuwa na moshi wa matairi yaliyochomwa moto uliochanganyika na hewa ya machozi iliyopigwa kwa mabomu ya polisi.