Watuhumiwa ubadhirifu Moro waanza kuonja joto ya jiwe

Muktasari:

  • Mkurugenzi wa Halmashauri ya Gairo, Agnes Mkandya alisema jana kuwa uamuzi huo umefikiwa na ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro  baada ya kuundwa tume maalumu kuchunguza tuhuma  hizo.

Gairo. Watumishi wanane wa Halmashauri ya Wilaya Gairo wamesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi baada ya kutuhumiwa kuhusika katika ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za miradi ya maendeleo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Gairo, Agnes Mkandya alisema jana kuwa uamuzi huo umefikiwa na ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro  baada ya kuundwa tume maalumu kuchunguza tuhuma  hizo.

“Nilipofika Gairo bosi wangu wa mkoa (RAS) aliniuliza kama watumishi wanaotakiwa kusimamishwa kupisha uchunguzi walishakabidhiwa barua zao, nikamweleza kuwa bado na amenitaka niwakabidhi kulingana na maelekezo,” alisema.

Mkurugenzi huyo aliwataka watumishi katika halmashauri hiyo kufanya kazi kwa weledi na kuacha kutumia fedha za miradi ya maendeleo inayopitia katika idara zao tofauti na maelekezo.

Alisema endapo atabaini kuwapo kwa mianya ya matumizi mabaya ya fedha, hatamfumbia macho mtu.