Watumishi 8 Gairo wasimamishwa kazi kwa ubadhirifu

Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro ,Dkt John Ndunguru.

Muktasari:

Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro ,Dkt John Ndunguru amewasimamisha kazi watumishi nane wa Halmashauri ya Wilaya Gairo kupisha uchunguzi kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za miradi ya maendeleo.

Gairo. Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro ,Dkt John Ndunguru amewasimamisha kazi watumishi nane wa Halmashauri ya Wilaya Gairo kupisha uchunguzi kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za miradi ya maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkurugenzi wa Halmashauri ya Gairo, Agnes Mkandya alisema uamuzi huo ulifikiwa na ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, kufuatia tume maalum iliyoundwa kuchunguza tuhuma katika halmashauri hiyo,kwa maelekezo ya Waziri wa Tamisemi baada ya tuhuma za ubadhirifu wa fedha.
Alisema barua za kusimamishwa kazi kwa watumishi hao zilitumwa kwa mkurugenzi wa awali wa Gairo Mbwana Magotta,(aliyeachwa kwenye uteuzi) na katibu Tawala wa mkoa wa Morogoro Dk John Ndunguru,ikiwa ni miezi kadhaa baada ya kuundwa kwa tume hiyo maalum na mkuu wa Mkoa wa Morogoro  ili kuchunguza madai mbalimbali ya madiwani wa wilaya hiyo,ikiwa ni maelekezo ya waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na maelekezo hayo kuwasilishwa kwa mkuu wa mkoa wa Morogoro na Katibu mkuu Wizara ya Tawala za mikoa na Serikali za mitaa Tamisemi,Musa Ibrahim Iyombwe.
Mkurugenzi aliyeondoka,Magotta,ambaye hakuwakabidhi walengwa hivyo alipoteuliwa kushika wadhifa huo aliagizwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro,Dk John Ndunguru kukabidhi barua hizo kwa walengwa.
“Nilipofika Gairo bosi wangu wa mkoa RAS aliniuliza kama watumishi wanaotakiwa kusimamishwa ili kupisha uchunguzi walishakabidhiwa barua zao nikamweleza walikuwa bado na kunitaka niwakabidhi kulingana na maelekezo,”alisema
Aliwataja watumishi waliosimamishwa ni kutoka idara za Afya,Elimu,Mipango na Fedha ambao ni Tumaini Njelela,Godlover Nnko, Josephat Dyambo, Rajabu Mushi, Mustafa Kachechele, Willy Chiwayu, Edward Mkumbo na Karimu Sululu.
Aidha mkurugenzi huyo aliwataka watumishi katika halmashauri ya wilaya ya Gairo  kufanya kazi kwa weledi na kuacha kutumia fedha za miradi ya maendeleo inayopitia katika idara zao tofauti na maelekezo ambapo alisema endapo atabaini kuwapo kwa mianya yeyote ya matumizi mabaya hatafumbia macho mtumishi husika.
Miezi miwili iliyopita ikiwemo Aprili 15 na Mei 7 mwaka huu vikao vya baraza madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Gairo kwa nyakati tofauti vilizimia kutokuwa na imani na aliyekuwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo Mbwana Magotta kutokana na kushindwa kusimamia ipasavyo miradi ya maendeleo yenye thamani ya shilingi 995 milioni.
Vikao hivyo chini ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo Rachel Nyangasi,viliazimia kusimamishwa kwa Mkurugenzi huyo na kupeleka mapendekezo yake kwa mamlaka inayohusika kwa mkuu wa mkoa na katibu tawala mkoa Morogoro ambapo mamlaka hizo ziliunda tume ya uchunguzi huku mkurugenzi huyo akiendelea na shughuli zake za kikazi.
Mwenyekiti huyo katika taarifa yake alitoa mifano kadha   ya miradi iliyoshindwa kutekelezwa, au kutekelezwa chini ya kiwango ukiwemo mradi wa ujenzi wa barabara   ya  Chakwale-Leshata, Gairo-Rubeho-Kisitu, Iyogwe-Chogohale, Ndege  -Mandege, Gairo-Nongwe, na Chagongwe-Lufikili,ambapo  kiasi cha  Shilingi 995 milioni zilitumika  lakini  hali  ya barabara  hizo  ni mbaya.
Aidha mwenyekiti wa halmashauri hiyo alidai kuwa  fedha  za  miradi  ya  barabara  zilitumika katika mazingira ya  udanganyifu hivyo kufanya wao kama madiwani kutoridhishwa nayo.
Mbali na miradi ya barabara,pia alitolea  mfano mradi wa maji  katika  vijiji   kumi  katika wilaya hiyo ambavyo  ni Iyenje,Itaragwe,Idibo,Iyogwe,Kilama ,Ndogomi,Kitaita,Leshata, Chogohali na Makuyu ambao  umegharimu shilingi 229 milioni lakini  mpaka  sasa hakuna  hata  kijiji kimoja kilichopata maji  katika  mradi  huo.
Madiwani hao pia awali walisusia kabisa kufanya kazi na Magotta,kabla ya Tamisemi kuagiza waendelee kufanya naye kazi wakati Tume ikiundwa na mkoa na kuendelea na uchunguzi,walilalamikia kutoitishwa kwa vikao halali vya Halmashauri na kunyimwa fursa ya kukagua miradi ya maendeleo  inayotekelezwa.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Gairo Ahmed Shabiby alisema wilaya ya  Gairo imekuwa na miradi mbalimbali  ya maendeleo ikiwemo ya Afya,Maji,Elimu na mingineyo mingi lakini imekuwa ikitumka vibaya na kila madiwani wanapohoji majibu yasiyoeleweka hutolewa na watendaji jambo linaloifanya kuendelea kuwa nyuma kimaendeleo.
Mwisho..