Watumishi hewa waendelea kuvuta mishahara

Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella

Muktasari:

Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema baada ya kubainika mtumishi ambaye alikataa kumtaja jina wala idara anayofanyia kazi ili kuepuka kuharibu uchunguzi unaoendelea, aliwataja wenzake wengine ambao pia wanaendelea kulipwa mishahara.

 Wakati Serikali ikitangaza kuwaondoa kazini watumishi hewa zaidi ya 19,000, mkoa wa Mwanza umebaini kuwapo watu waliomo kwenye orodha ya watumishi hewa wanaoendelea kulipwa mishahara bila kuwa kazini.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema baada ya kubainika mtumishi ambaye alikataa kumtaja jina wala idara anayofanyia kazi ili kuepuka kuharibu uchunguzi unaoendelea, aliwataja wenzake wengine ambao pia wanaendelea kulipwa mishahara.

Katika operesheni dhidi ya watumishi hewa, mkoa wa Mwanza ulibainika kuwa na watumishi 1,057 waliokuwa wakiigharimu Serikali zaidi ya Sh2.1 bilioni kwa mujibu wa Mongella.

Akizungumza na wadau wa elimu katika ukumbi wa mikutano ofisini kwake juzi, Mongella alisema kitendo cha kumbaini mtumishi hewa huyo kimeisukuma sekretarieti ya mkoa huo kuanza upya uhakiki wa majina na malipo ya mishahara kwa watumishi wote wa umma mkoani Mwanza. “Baada ya uchunguzi na uhakiki upya kukamilika, tutatoa taarifa kamili ya idadi, majina na hasara ya fedha walizoisababishia Serikali,” alisema.

Mkazi wa Mabatini jijini hapa, Lule Boniface alisema kwa kuwa Serikali iliahidi uhakiki wa watumishi ni vyema jukumu hilo likaendelea bila kukoma.

Kuhusu uhamisho na upandishwaji wa madaraja walimu kuwa maofisa elimu kata, mkuu huyo wa mkoa aliiagiza idara ya elimu kuhakikisha suala hilo linazingatia uwiano wa walimu kwa kila eneo.

Awali, mdau wa elimu kutoka wilayani Sengerema, Alex Masasi aliibua hoja ya baadhi ya shule wilayani humo kukabiliwa na upungufu wa walimu baada ya waliokuwapo kuhamishwa au kupandishwa ngazi kuwa maofisa elimu wa kata.

Mongella alimuagiza ofisa elimu mkoa wa Mwanza, Michael Lugola kuitisha kikao cha pamoja cha walimu wakuu, Chama cha Walimu Tanzania (CWT) mkoa na wadau wengine ili kujadili na kutafutia ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili sekta ya elimu kwa ajili ya kuongeza ufanisi na kujenga uhusiano mwema kazini.