Thursday, November 9, 2017

Watumishi wapya 2,088 waajiriwa kada ya afya

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi hmakweta@mwananchi.co.tz

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeajiri watumishi wapya 2,088 wa kada mbalimbali za afya.

Kati ya watumishi hao 30 wanakwenda wizarani na 2,058 wameitwa kazini kupitia Wizara ya Tamisemi ambao wanakwenda kutoa huduma za afya katika hospitali za mikoa, halmashauri na taasisi mbalimbali.

Tangazo hilo lililotolewa jana limekuja wiki moja baada ya Tamisemi kusitisha ajira mpya zilizoombwa kwa kipindi cha Agosti.

Alipoulizwa sababu za kusitishwa awali kwa zoezi hilo, kaimu msemaji wa Wizara ya Afya, Catherine Sungura alisema halikuwa suala la wizara hiyo bali lilifanywa na Tamisemi. “Sisi tumetoa majina 30 tu kwa waajiriwa wa Wizara ya Afya, majina mengine 2,058 yalitolewa jana (juzi) na Tamisemi,” alisema Sungura.

Taarifa iliyotolewa jana na kitengo cha mawasiliano serikalini afya kupitia ofisa huyo ilieleza kuwa Wizara ya Afya ilipokea kibali cha kuajiri watumishi 3,152 ambacho kilikuwa kwa ajili ya wizara, hospitali za mikoa, halmashauri na taasisi mbalimbali.

“Waombaji 30 wamechaguliwa na kupangiwa ajira Wizara ya Afya na 2,058 wamechaguliwa katika hospitali za mikoa na halmashauri majina yao yametangazwa kwenye tovuti ya Tamisemi,” ilisema taarifa hiyo. Ilieleza kuwa waombaji wote waliochaguliwa wanatakiwa kuripoti Wizara ya Afya mjini Dodoma katika muda wa siku 14 kuanzia jana kwa ajili ya kukamilisha taratibu za ajira Serikalini.

Oktoba 31, Tamisemi ilisitisha ajira hizo kwa walioitwa kazini na kuwataarifu waajiri na waombaji wote wa ajira za kada za afya kuwa imesitisha kwa muda mfupi.

-->