Watumishi watano waisoma namba Manyoni

Muktasari:

Taarifa ya Ofisa habari wa halmashauri hiyo, Veronica Luhaga imesema Mwambe amewaweka kando watumishi hao kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao vizuri, uzembe na utovu wa nidhamu.

Manyoni. Ni msemo uleule wa kuisoma namba leo umewakumba watumishi watano wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni baada ya kusimamishwa kazi na Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Geoffrey Mwambe.

Taarifa ya Ofisa habari wa halmashauri hiyo, Veronica Luhaga imesema Mwambe amewaweka kando watumishi hao kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao vizuri, uzembe na utovu wa nidhamu.

Mwambe amefanya uamuzi huo kwenye mkutano na wafanyakazi wa halmashauri uliofanyika Manyoni leo.

Watumishi hao ni Mkuu wa Idara ya Ugavi, Genesius Rugemalira, Daktari John Amita wa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni, Muuguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni, Mika Iloti, Msaidizi wa ofisi, Anthony Sanga na Mtendaji wa Kijiji cha Makasuku, Mussa Ndahan.

Mkuu wa Wilaya amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kuwasimamisha mara moja moja kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili.