Wauza ngozi wa Tanzania walilia soko la Kenya

Muktasari:

  • Wakizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, baadhi ya wafanyabiashara wa ngozi Manispaa ya Musoma wameiomba Serikali kulegeza masharti kwa kuruhusu usafirishaji wakati mchakato wa kufufua na kuanzisha viwanda vya ngozi ukiendelea.

 Baada ya Serikali kupiga marufuku usafirishaji wa ngozi nchi ya nchi, wafanyabiashara wa bidhaa hiyo mkoani Mara wameanza kulia njaa kwa kukosa soko la uhakika la ndani.

Wakizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, baadhi ya wafanyabiashara wa ngozi Manispaa ya Musoma wameiomba Serikali kulegeza masharti kwa kuruhusu usafirishaji wakati mchakato wa kufufua na kuanzisha viwanda vya ngozi ukiendelea.

Mfanyabiashara wa ngozi, Alex Mafuru alisema siyo sahihi kuzuia uuzwaji wa ngozi nje ya nchi wakati hivi sasa hakuna kiwanda cha kuchakata na kusindika ngozi mkoani Mara na mikoa mingine jirani kama Mwanza na Simiyu.

Robert Magori alisema kuruhusu biashara halali ya ngozi nje ya nchi kipindi hiki wakati Taifa likijipanga kuingia kwenye uchumi wa viwanda ifikapo 2025, siyo tu kutalinda mitaji yao, bali pia kitaiongezea Serikali mapato kupitia kodi na ushuru mbalimbali.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo (TCCIA), Mkoa wa Mara, Boniphace Ndengo alisema kabla ya zuio la Serikali asilimia 70 ya ngozi inayozalishwa mkoani humo ilikuwa ikiuzwa nchini Kenya.

Ofisa mfawidhi wa zao la ngozi Manispaa ya Musoma, Swalehe Twalibu alisema tayari halmashauri hiyo imepeleka ombi maalumu Wizara ya Viwanda na Biashara ili wafanyabiashara mkoani Mara waruhusiwe kusafirisha nje ya nchi bidhaa hiyo hadi hapo mchakato wa kuanzisha viwanda vya kusindika ngozi utakapokamilika.

Kwa siku, Manispaa ya Musoma huzalisha ngozi 25 za ng’ombe na 10 za mbuzi na kondoo ambazo hazina soko kwa sasa kutokana na Serikali kupiga marufuku uuzaji wa bidhaa hiyo nje ya nchi tangu mwaka 2016.

Kabla ya zuio, soko kubwa la bidhaa hiyo lilikuwa nchini Kenya ambako kuna viwanda vingi vya ngozi.