Breaking News
Thursday, January 11, 2018

Wavuliwa uongozi kwa kugeuza madarasa kuwa migodi ya almasi

 

By Suzy Butondo, Mwananchi mwananchipepers@mwananchi.co.tz

Shinyanga. Uongozi wa Kijiji cha Maganzo umevunjwa baada ya kubainika kuruhusu kuchimba madini ya almasi ndani ya madarasa ya Shule ya Msingi ya Jitegemee wilayani Kishapu na hivyo kuhatarisha maisha na usalama wa wanafunzi na walimu wao.

Amri hiyo ilitolewa na mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu suala hilo wakati wa ziara ya kikazi inayoendelea katika wilaya za mkoa huo.

“Nimesikitishwa na kitendo cha viongozi walioaminiwa na kupewa dhamana ya kuongoza kugeuza vyumba vya madarasa kuwa migodi ya kuchimba madini kiasi cha kusababisha majengo hayo kuwa na nyufa,” alisema Telack.

“Nimevunja uongozi huu kuanzia leo (jana) kwa sababu wamekosa sifa za kuendelea kuwepo madarakani.”

Awali katibu msaidizi wa Baraza la Wazee wa Maganzo, George Mgashi alimuomba mkuu huyo wa mkoa kuvunja uongozi huo kutokana na kukabiliwa na tuhuma kadhaa, zikiwezo ubadhirifu wa fedha za maendeleo na kugeuza madarasa ya shule kuwa migodi ya almasi.

Hoja hiyo iliungwa mkono na mjumbe wa baraza hilo, Nyerere Masanja aliyeongeza kuwa uongozi huo umekuwa ukitoa maneno ya kejeli dhidi ya wananchi wanapohoji vitendo hivyo.

Katika ziara hiyo, Telack pia alikagua na kuelezea kutoridhishwa na ubora wa ujenzi choo chenye matundu 10 uliogharimu zaidi ya Sh33 milioni. Ili kujiridhisha na gharama halisi za mradi huo, mkuu wa mkoa alimwagiza mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Kishapu, Steven Magoiga, aliyekuwepo kwenye ziara yake, kutuma timu kukagua matumizi yote, kuanzia ujenzi wa choo na vyumba vya madarasa na kutaka watakaobainika kujihusisha na ubadhirifu, wachukuliwe hatua za kisheria.

-->