Wizara yaagiza madai ya wavuvi kuchunguzwa

Muktasari:

Wavuvi watatu wanadai kupokwa mtumbwi, leseni, simu na kisha kutoswa baharini.

Mafia. Naibu Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Abdallah Ulega amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Shaibu Anunduma kuunda kamati kuchunguza madai ya wavuvi watatu kupokwa mtumbwi, leseni, simu na kisha kutoswa baharini.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Agosti 2,2017 saa tano asubuhi baada ya kuvua samaki katika Kisiwa cha Mbarakuni kilichopo ndani ya Hifadhi ya Bahari (Marine Park) kinyume cha sheria.

Ulega ameagiza kuundwa kamati baada ya kutokea mvutano kati ya maofisa wa Hifadhi ya Bahari na wananchi wa Kijiji cha Jojo-Mafia wanaojishughulisha na uvuvi  wanaolalamika kwamba wananyanyaswa na maofisa hao.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana Jumanne Novemba 21,2017 katika Kijiji cha Jojo, mwenyekiti wa kijiji hicho, Mussa  Hassan alisema wavuvi Hamis Athuman, Hamad Faki na Issa Shali walitoswa baharini na waliokolewa na mvuvi wa kijiji kingine saa tisa alasiri ikiwa ni saa nne tangu walipotoswa.

Mwenyekiti huyo amesema wanakijiji  wanategemea shughuli za uvuvi katika Kisiwa cha Mbarakuni kuendesha maisha yao lakini wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili.

Kutokana na hali hiyo, Naibu Waziri Ulega amesema ni kosa la jinai kuwatosa baharini  wavuvi wanaokiuka sheria za uvuvi.

“Nchi inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, utaratibu na kanuni. Wavuvi wakikamatwa wanatakiwa kuletwa kwenye kamati ya kijiji na ikishindikana wanapaswa kupelekwa polisi. Mhalifu yeyote anapelekwa polisi,” amesema.

Amesema kamati itakayoundwa kuchunguza tukio hilo inapaswa kuwa huru ili itende haki.

Ulega amesema wanachotaka ni uhusiano mwema kati ya wahifadhi na wananchi na kwamba, maofisa watakaobainika kuwatosa baharini wavuvi hao watawajibishwa kwa mujibu wa sheria.

Pia, ameagiza wavuvi kufuata sheria akisema kisiwani hicho na vingine vya Shungimbili na Nyororo vimehifadhiwa kisheria hivyo hawapaswi kufanya shughuli za kibinadamu.

Mkurugenzi wa Hifadhi za Bahari, Dk Milali Machumu amekanusha wavuvi hao kutoswa baharini.

Amesema kabla ya tukio hilo, wavuvi hao waliwateka maofisa wao na kuwapeleka kijijini.