Wawili waamua kukatiza maisha kwa kujinyonga

Muktasari:

Kaimu Kamanda wa polisi Mkoa wa Kagera, Abel Mtangwa amesema matukio hayo yalitokea mwishoni mwa wiki iliyopita na kuwataja waliojiua kwa kujinyonga kuwa ni Aidan Gordian (20) na Amini Nuru (35).

Bukoba. Watu wawili katika Wilaya ya Muleba na Missenye mkoani Kagera, wamekufa kwa kujinyonga huku mmoja akiacha ujumbe wa maandishi unaodai kuchoshwa na manyanyaso.

Kaimu Kamanda wa polisi Mkoa wa Kagera, Abel Mtangwa amesema matukio hayo yalitokea mwishoni mwa wiki iliyopita na kuwataja waliojiua kwa kujinyonga kuwa ni Aidan Gordian (20) na Amini Nuru (35).

Mtangwa alisema Gordian, aliyekuwa   mkazi wa Kijiji cha Rubya Kata ya Kashasha wilayani Muleba, alikutwa amejinyonga kwa kutumia chandarua chumbani kwake, huku akiacha ujumbe uliosomeka kuwa amechoshwa na manyanyaso.

Alisema Nuru aliyekuwa mkazi wa kijiji cha Katare, tarafa ya Kiziba Wilaya ya Missenye, alikutwa amejinyonga kwa kutumia kipande cha shuka kwenye korido la nyumba yake.

Mtangwa alisema mbali na kutojua sababu za kifo hicho, hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo.