Wawili wafariki dunia katika matukio tofauti

Kamanda wa Polisi mkoani hapa,  Mponjoli Mwabulambo 

Muktasari:

Matukio hayo yametokea katika wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita


Nyang’hwale. Watu wawili wamefariki dunia wilayani hapa mkoani Geita katika matukio mawili tofauti.

Peter Sumuni (75) mkazi wa kijiji cha Ifugandi amekutwa amefariki dunia shambani kwake na  Mihayo Kurwa (57) mkazi wa kijiji cha Kaseme Nyang’hwale amejinyonga hadi kufa kwa kutumia kamba ya katani.

Akizungumza leo Julai 19, 2018 Kamanda wa Polisi mkoani hapa,  Mponjoli Mwabulambo amesema Sumuni amefariki dunia Julai 17, 2018 na  mwili wake kukutwa shambani huku ukiwa umezungushiwa kamba shingoni.

Amesema kabla ya kukutwa na umauti, alihudhuria sherehe ya kupokea mahali kwa jirani yake, alirejea nyumbani kwake akiwa amelewa na kutaka kumdhalilisha mkewe, Suzana Luponda.

 

 

“Mzee huyu alitaka unyumba kwa mkewe mbele ya watoto na wakwe zake, kulitokea vurugu na mkewe akaingia ndani na yeye (marehemu) kubaki nje. Inatia mashaka maana baada ya hapo  mwili wake ulikutwa shambani na hakuna mazingira yanayoonyesha kama alijinyonga,” amesema.

 

Amesema mzee huyo atakuwa ameuawa na kwamba watu watano wa familia hiyo wanashikiliwa na polisi kwa uchunguzi.

 

Kuhusu Kurwa, kamanda Mwabulambo amesema alijinyonga kwa kutumia kamba ya katani.

 

Amesema marehemu hakuacha ujumbe wowote na kubainisha kuwa alikuwa akisumbuliwa na  ugonjwa wa kifafa.

 

Katika tukio jingine, kamanda huyo amesema mwishoni mwa wili iliyopita katika kijiji cha Kasuguya mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Nkala (55), alimbaka mtoto mwenye umri wa miaka saba.

Amesema mtuhumiwa huyo alikua kibarua kwenye mashamba ya mpunga ya Maganga Makaranga ambaye ni baba mzazi wa mtoto.

 

“Siku hiyo Makaranga  walimpa mtoto huyo chakula ampelekee Nkala. Baada ya kukaa  muda mrefu bila kumuona mwanae aliamua kumfuatilia na kumkuta  akiwa mtupu pamoja na mtuhumiwa,” amesema kamanda.

 

Amesema uchunguzi unaonyesha kuwa mtoto huyo alibakwa, kwamba mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani.