Thursday, January 11, 2018

Wazazi wanawakwaza wanafunzi kufanya vizuri mitihani ya mwisho

 

By Faustine Fabian, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

 Ufaulu mdogo wa wanafunzi wa darasa la saba mwaka 2017 katika Shule ya Msingi Mabambasi wilayani hapa, umechangiwa na baadhi ya wazazi kuwazuia watoto wao kufanya vizuri ili waishie kuolewa au kuchunga mifugo.

Hali hiyo imesababisha shule hiyo kuwa ya mwisho kiwilaya ambapo kati ya wanafunzi 20 waliohitimu, hakuna hata mmoja aliyefaulu kuendelea na elimu ya sekondari.

Akizungumza kwenye kikao cha wazazi na wadau wa elimu shuleni hapo, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Samson Tingo alisema matokeo ya darasa la saba yamekuwa yakishuka kila mwaka ambapo mwaka 2013 walihitimu wanafunzi 29 na aliyefaulu ni mmoja. “Halikadhalika mwaka 2015 walihitimu wanafunzi 21 akafaulu mmoja, 2016 walihitimu 19 wakafaulu wanne na mwaka huu 2017 walihitimu 20 hakuna aliyefaulu. Hii ni dhahiri kuwa jamii ya watu hawa ambao wengi ni wafugaji wanawazuia watoto wao kufanya vizuri ili wawasaidie kuchunga kisha kujipatia urithi wa mifugo badala ya elimu,” alisema.

Kaimu ofisa elimu Wilaya ya Meatu, John Mpamwa alisema inashangaza wanafunzi wote wafeli wakati kwenye mtihani wa ‘mock’ walifaulu kwa alama za juu.

“Baada ya matokeo kutangazwa, niliita wanafunzi saba na kuwapa mtihani wa majaribio wote walifaulu,” alisema Mpamwa.

Mmoja wa wazazi, Dotto Miligwa alikiri kuwepo kwa wazazi wanaowashawishi watoto wasifanye vizuri kwa sababu ya kuolewa ama kuchunga mifugo.

Mwenyekiti wa kijiji cha Mwamanimba alisema jamii hiyo haina mwamko wa elimu, lakini kupitia matokeo hayo amejipanga kuhakikisha mwaka ujao wanafunzi wanafaulu. Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Fabian Manoza alisema jamii wilayani humo ni ya wafugaji ambao wanaona kuwa kumpeleka mtoto shule aache kuchunga ni kupoteza muda.

Shule ya Msingi Mabambasi imeshika pia nafasi ya mwisho kimkoa kati ya shule 8,645.     

-->