Serikali yatangaza msako wa wazazi

Muktasari:

Yasema kuwa wanakwamisha malengo na mikakati ya Taifa

Serikali imetangaza msako kwa wazazi walioshindwa kwa makusudi kuwapeleka watoto wao kuanza shule ya msingi kwani wanakwamisha malengo na mkakati wa Taifa.

Wito huo ulitolewa jana Machi 17, 2018  na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais (Tamisemi) anayeshughulikia Elimu, Tixon Nzunda na kubainisha kuwa kundi hilo ndilo linalosababisha kuwepo kwa ujambazi na vibaka wengi katika maeneo ya mijini hususan katika miji mikuu.

Nzunda alitoa kauli hiyo wakati akifungua warsha ya siku moja kwa maofisa elimu, maendeleo ya jamii, wadhibiti ubora wa elimu na viongozi wa kisiasa kutoka halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam iliyotolewa na Mtandao wa Elimu Tanzania (MET).

Kiongozi huyo amesema mpango wa MET unakwenda sambamba na malengo ya Serikali ya kuwasaidia vijana waliokosa elimu hasa katika maeneo ya mijini ambao wakikosa elimu ya kuwafaa katika maisha yao hugeuka kuwa maadui wa maendeleo.

Amewataka MET kutanua wigo zaidi kwa kuwa tatizo hilo ni kubwa na bila ya kulisimamia kwa nguvu zote, Tanzania itajenga kizazi kisichokuwa na mwelekeo mzuri hata katika sura za kimataifa.