Wazee waliomkosoa Rais Mugabe watiwa mbaroni

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe

Muktasari:

Kwa mujibu wa Jumuiya ya Mawakili wa Haki za Binadamu Zimbabwe, Mahiya ambaye ni msemaji wa chama cha maveterani alikamatwa na kuzuiliwa baada ya kujisalimisha katika kituo cha polisi.

Harare, Zimbabwe. Polisi nchini Zimbabwe inawashikilia mashujaa wawili wa vita vya uhuru nchini humo kwa tuhuma za kutamka   kuwa Rais Robert Mugabe ni dikteta na kumtaka ajiuzulu.

Maveterani hao, Victor Matemadanda na Douglas Mahiya wanatuhumiwa kukiuka sehemu ya 22 ya sheria ya nchi inayotaka kuheshimiwa Serikali iliyochaguliwa kwa mujibu wa Katiba na sehemu ya 33 inayokataza kuvunjiwa heshima ofisi ya Rais.

Kwa mujibu wa Jumuiya ya Mawakili wa Haki za Binadamu Zimbabwe, Mahiya ambaye ni msemaji wa chama cha maveterani alikamatwa na kuzuiliwa baada ya kujisalimisha katika kituo cha polisi.

Imesema Matemadanda ambaye ni katibu mkuu wa chama cha maveterani alikamatwa jana na maofisa wa polisi nyumbani kwake katika Mkoa wa Midlands na kupelekwa kituo cha polisi mjini Harare.