Waziri Jafo aagiza uongozi Sekondari Jangwani kufumuliwa, aonya wanafunzi

 Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo


Muktasari:

  • Waziri aliwataka viongozi wa mkoa kuangalia suala la walimu waliokaa kwa muda mrefu shuleni hapo.

Dar es Salaam. Isingepita hivi hivi tu. Kitendo cha shule ya wasichana ya Jangwani kuwa miongoni mwa shule za mwisho kimeondoka na watu.

Matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa hivi karibuni na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), yamewaingiza matatani walimu na uongozi wa shule hiyo.

Akizungumza jana alipotembelea shule hiyo, Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo aliagiza yafanyike mabadiliko ya kiuongozi na walimu.

Jafo alimuagiza katibu tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mbando hadi kufikia leo awe amechukua hatua na kubadilisha uongozi wa shule hiyo.

“Fanya mabadiliko katika uongozi na walimu, na ukijiridhisha kuna mwalimu ni tegemeo kubwa la wanafunzi mbakize Jangwani,” alisema Jafo na kupigiwa makofi na wanafunzi.

Jangwani ni miongoni mwa shule zilizoshika mkia katika matokeo ya kidato cha sita yaliyotolewa Julai 13.

“Fanyeni mabadiliko ya walimu hawa, haiwezekani mwalimu mmoja akakaa miaka mitano bila kuhamishwa kituo cha kazi,” alisema.

“Wale wengine waondolewe haraka tena ufanye kwa haki, badilisha uongozi na uwapeleke maeneo mengine.”

Waziri huyo aliwataka viongozi wa mkoa kuangalia pia suala la walimu waliokaa kwa muda mrefu shuleni hapo.

Alisema shule hiyo ilikuwa na sifa kubwa kitaifa na ilikuwa ni ndoto ya kila msichana.

“Shule yenye upako maalumu na sifa na tunu kwa nchi yetu, lakini leo hii imekuwa ya tatu kutoka mwisho,” alisema na kuongeza:

“Shule kuwa ya 451 wakati shule ya mwisho ni ya 453, ninyi mna unyafu wa kitaaluma shuleni. Mtoto asipokuwa vizuri kiafya anakuwa na unyafuzi.”

Jafo alisema licha ya Jangwani kuwa na walimu 87, lakini imeshindwa na shule ya Sekondari ya Kibaha yenye walimu 57.

“Shule ya Jangwani hali yenu ni mbaya, haiwezekani Jangwani mkapata ‘division one’ moja hata Biharamulo kule Ngara wamepata saba,” alisema waziri huyo.

“Yaani nyinyi mwendokasi mnaiona inapita halafu mnapata one moja kweli? Mkuu wa wilaya (Sophia Mjema) shule hii imetutia aibu na wewe umesoma hapa.”

Alitaka kila mmoja atimize wajibu wake wakiwamo wanafunzi na kuwaonya wanafunzi wanaoangalia mitandao ya kijamii na picha zisizofaa na wale wanaojihusisha na uasherati.

Ndalichako aililia

Jafo hakuwa pekee yake aliyesikitishwa na matokeo hayo ya Jangwani, waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako alisikitishwa na matokeo ya shule hiyo na kusema yanakatisha tamaa.

Profesa Ndalichako aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa mfuko wa kukuza ujuzi kwa vijana wanaosoma vyuo vikuu na vyuo vya ufundi katika fani mbalimbali unaolenga kuboresha teknolojia katika sekta ya viwanda.

“Serikali imekuwa ikifanya juhudi nyingi za kuhakikisha shule na vyuo vyetu vinafanya vizuri. Tumefanya uwekezaji wa kutosha katika vyuo na hata shule za msingi na sekondari ikiwamo Shule ya Jangwani ambayo imeshika mkia,” alisema.

Alisema Serikali inapenda kuona matokeo mazuri katika maeneo ambayo inafanya uwekezaji mkubwa, lakini ikitokea yanakuwa kinyume yanakatisha tamaa.

“Nimesikitishwa na Shule ya Jangwani kushika mkia, ni shule ambayo nimekwenda pale si mara moja wala mara mbili, tumefanya uwekezaji mkubwa katika shule hiyo. Ukienda pale mazingira na miundombinu ya shule ni ya kuridhisha, lakini imeshika mkia,” alisema.

Akizindua mfuko wa kukuza ujuzi alisema wizara yake kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (Tea)imeanzisha mfuko huo kupitia taasisi za elimu ya juu na vyuo vya ufundi unaolenga kuboresha na kukuza ujuzi, hususan kwa vijana wanaosoma vyuo mbalimbali ili kukuza sekta ya viwanda.

“Mfuko huu unalenga kuviwezesha vyuo vyetu vikuu na vyuo vya ufundi na mafunzo kutoa elimu iliyo bora itakayosaidia vijana wetu kutoka na ujuzi utakaosaidia kukuza sekta yetu ya viwanda,” alisema.