Waziri Kigwangala atua kijiji walichokufa Simba tisa, aamuru wafugaji eneo hilo wahame

Muktasari:

Awatuhumu wafugaji wanaoishi kijijini hapo kuhusika na mauaji ya simba hao.


Serengeti. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangala ameagiza wafugaji wanaoishi eneo la malisho katika kijiji cha Nyichoka wilayani hapa kuhama mara moja.

Akiwa eneo ambalo simba tisa waliuawa kwa sumu Mei 31 katika eneo la malisho ya kijiji cha Nyichoka, Dk Kigwangalla amesema wafugaji wanaoishi maeneo hayo ndiyo waliohusika na hujuma hiyo.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo leo Julai 17, DK Kigwangala amesema wavamizi hao wanatakiwa kuondoka kuanzia sasa kwa kuwa kijiji hicho kimepimwa na kina mpango wa matumizi bora ya ardhi.

“Hapa ninyi ni wanufaika wakubwa wa uhifadhi kwa kuwa ninyi mnaunda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Ikona, eneo la malisho mmekaribisha wafugaji hatuwezi kukubali kubadili matumizi ya mpango ambao umewawezesha kuunda jumuiya hii," amesema.

Ameagiza taasisi zote za uhifadhi kutumia sheria ya kutaifisha mifugo inayokamatwa ndani ya hifadhi, badala ya kupiga faini ili kukomesha wanaochungia ndani ya maeneo hayo.

"Ukilea nyani utavuna mabua na sisi sasa tunatakiwa tubadilike kwani tumekuwa wapole, wameteketeza familia nzima ya simba ambao wana mchango mkubwa wa uchumi,"amesema na kuongeza:

“Sitakubali simu za wabunge, mwenyekiti au katibu wa CCM kwa hili. Kama mnatafuta kura hizi hazifai maana chama chetu hakikubaliani na hujuma kama hizo.”

Amesema maliasili inachangia zaidi ya asilimia 17 ya pato la taifa na mifugo inachangia asilimia nne.

“Kwa mtu mwenye akili lazima awekeze kwenye pato kubwa. nasema tena sasa ni mwendo wa kutaifisha ili tuweze kulinda maliasili tuliyopewa na Mungu kuitunza,”amesema.

Awali, mkurugenzi wa uhifadhi wa Shirika la Hifadhi la Taifa (Tanapa), Martin Loibooki amesema chanzo cha migogoro katika maeneo ya hifadhi ni kushindwa kusimamia kanuni za uendeshaji ikiwamo usimamizi wa matumizi bora ya ardhi.

Naye mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu ameagiza kufikia Agosti 15 wafugaji wote wanaoishi maeneo ya malisho wawe wameondoka.

"Waziri hili niachie mwenye akili aanze kuondoka kuanzia sasa, kwa kuwa itakapofika muda huo itakuwa uvungu kwa uvungu nyumba kwa nyumba aliyekuuzia eneo mtajuana wenyewe," amesema.