Waziri Lukuvi anusa ufisadi wa viwanja CDA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi 

Muktasari:

Pia, ametangaza kiama kwa madalali wa mahakama nchi nzima, ambao wamekuwa wakiuza nyumba na viwanja vya wananchi kwa njia ya mnada siku za mapumziko na sikukuu, kuwa dawa yao inachemka.

Dodoma. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, jana aliwaweka rehani waliokuwa watumishi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA), akihoji vilipo viwanja 34,000.

Pia, ametangaza kiama kwa madalali wa mahakama nchi nzima, ambao wamekuwa wakiuza nyumba na viwanja vya wananchi kwa njia ya mnada siku za mapumziko na sikukuu, kuwa dawa yao inachemka.

Waziri Lukuvi alitoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma jana, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2017/2018 na aliomba kuidhinishiwa Sh70.7 bilioni.

Kati ya fedha hizo, Sh43.3 bilioni ni kwa ajili matumizi ya kawaida, Sh25.4 bilioni za miradi ya maendeleo na Sh2.1 bilioni ni kwa ajili ya Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi.

“Tunafahamu kulikuwa na viwanja vilivyopimwa CDA karibu 60,000 lakini hati zilizotolewa ziko 26,000 tu. Wale CDA wa zamani watatwambia hivi viwanja 34,000 viko wapi,” alisema Waziri Lukuvi.

Waziri Lukuvi alishangazwa na kuwapo kwa uhaba wa viwanja katika Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, wakati viwanja vilivyopimwa ni 60,000 na kuwaonya madalali waliohodhi viwanja hivyo.

“Viwanja 34,000 viko kwenye maduka ya madalali na watu fulani na uhakiki utafanywa kuhakikisha viwanja vyote 60,000 vinaingia mikononi mwa wananchi,” alisisitiza Lukuvi na kuongeza:

“Tunaomba maofisa wote wa CDA wamsaidie mkurugenzi na wale wote watakaojiingiza katika udanganyifu, kudhulumu, kutapeli au kuficha viwanja watachukuliwa hatua kali za sheria”.

“Nawatahadharisha sana hao madalali wafunge maduka yao ya kuuza viwanja kwa sababu sasa biashara ya kutoa viwanja imehamia sehemu mbaya zaidi”.

Waziri Lukuvi alisema kuanzia Julai 1, Serikali itaanza uhakiki wa umiliki wa viwanja vyote katika Manispaa ya Dodoma, na kutoa hati mpya kwa wamiliki zenye umri wa miaka 99.

“Kwa hiyo kila aliye na hati atakuta tangu amepewa ina miaka 33 leo imebaki miaka 10 aongeze miaka 66 hii imetolewa na Rais ili hati za Dodoma zifanane na hati nyingine Tanzania,”alisema.

Hata hivyo, alisema pamoja na kazi hiyo ya kubadilisha hati, haki za taasisi za fedha yakiwamo mabenki zitalindwa kulingana na mikataba iliyotumika kutoa mikopo na miamala mingine ya fedha.

“Tunajua wame- mortgage (waliweka viwanja kama dhamana). Mabenki hayatapata hasara. Tutafanya kazi vizuri ili mabenki yasipoteze haki yao kutokana na mabadiliko haya ya hati,”alisisitiza Waziri Lukuvi.

Waziri Lukuvi pia aliliarifu bunge kuwa Serikali iko katika hatua za mwisho za kupeleka muswada bungeni ili kuwadhibiti madalali wa mahakama wanaowaonea wananchi kwa mgongo wa amri za mahakama.

“Tutaleta sheria hapa bungeni ili kiwe kiama cha madalali wanaouza nyumba za wananchi siku za Jumamosi, Jumapili na siku za sikukuu kwa kivuli cha mahakama,”alisema.

Waziri Lukuvi aligusia yatakayokuwamo katika sheria hiyo kuwa ni pamoja na kuanisha sifa ya dalali na kupiga marufuku kuendesha minada siku za mapumziko.

“Nataka pia niwaonye watu wanaotumia ardhi kutakatisha fedha. Watu wanamiliki ardhi kubwa pasipo sababu. Kuna mmoja kule Lindi anamiliki hekta 4,000 kwenye ufukwe wa bahari. Nimezifuta”.

Waziri Lukuvi alisema ardhi yote iliyopo maeneo ya mjini ambayo haijapimwa, itapimwa na kuhakikiwa ili wamiliki wake walipe kodi ambayo hawailipi kwa mgongo kuwa maeneo yao hayajapimwa.

Mbali na suala hilo, alisema Serikali pia inakusudia kuongeza viwango vya pango la ardhi kutoka Sh400 hadi Sh800 kwa ekari kwa mwaka, kuanzia Julai Mosi mwaka huu.

Waziri Lukuvi, ameliambia Bunge kuwa ongezeko hilo litahusu mashamba ya biashara yaliyopimwa na kumilikishwa nje ya mji, ambayo yamekuwa hayalipi kodi.

Alisema kiwango kinachotozwa sasa cha Sh400 kwa ekari moja bado ni kidogo ikilinganishwa na thamani pamoja na uwezo wa uzalishaji wa ardhi husika.

Pia, Serikali inakusudia kupunguza tozo ya mbele (premium) kutoka asilimia 7.5 hadi asilimia 2.5 ya thamani ya ardhi kuanzia Julai mwaka huu.

“Ada hii hutozwa mara moja tu wakati wa umilikishaji wa ardhi kwa mujibu wa fungu la 31 la Sheria ya Ardhi namba 4 iliyopitishwa na Bunge mwaka 1999,” alisema.

Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, kupunguzwa kwa kiwango cha tozo ya mbele kutavutia wananchi wenye maeneo ya ardhi kujitokeza kwa wingi zaidi kupimiwa ardhi na kumilikishwa ardhi yao.

Wakati huohuo, wizara hiyo imeboresha muundo wa ofisi za Ardhi za Kanda, kwa kuanzisha kanda mpya ya Simiyu, kupunguza na kuongeza mikoa katika baadhi ya kanda.

Waziri Lukuvi alisema kuanzia Julai Mosi, Ofisi za Ardhi za Kanda zitakuwa zikihudumiwa mikoani ambapo Kanda ya Dar es Salaam itahudumia mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Kanda zingine ni Kanda ya Nyanda za Kusini ambayo ni mikoa ya Mbeya, Njombe, Rukwa na Songwe na Kanda ya Kati itakayohudumia mikoa ya Dodoma, Singida, Iringa na Morogoro.

Chini ya muundo huo, kanda nyingine ni ya Kaskazini ambayo ofisi itakuwa Arusha na itahudumia mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara na Kanda ya Ziwa yenye mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera.

Kanda nyingine kwa mujibu wa Lukuvi ni ya Kusini yenye mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma na Kanda ya Simiyu itakayohudumia mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara.

Alisema kwa mwaka 2017/2018, Wizara yake kwa kushirikiana na Halmashauri mbalimbali nchini, itaandaa hati miliki za ardhi 400,000, vyeti vya ardhi za vijiji 1,000 na za kimila 57,000.