Waziri Lukuvi atoa neno kuhusu Sheria ya Ardhi

Muktasari:

  • Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku moja tangu Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kusema kwamba marekebisho ya sheria hiyo, sura ya 113 kifungu cha 45 iwapo yatapitishwa na Bunge yataathiri mfumo wa rehani ya miliki ya mashamba nchini.

 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema kama kuna mtu ana maoni kuhusu kipengele chochote cha marekebisho ya Sheria ya Ardhi ayapeleke Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Mazingira yafanyiwe kazi.

Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku moja tangu Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kusema kwamba marekebisho ya sheria hiyo, sura ya 113 kifungu cha 45 iwapo yatapitishwa na Bunge yataathiri mfumo wa rehani ya miliki ya mashamba nchini.

“Huo ndio utaratibu, kwa hiyo kama kuna malalamiko yoyote yanayohusu marekebisho ya sheria hii basi ni vizuri yawahishwe wakati huu vikao vinapoendelea yatachambuliwa,” alisema Waziri Lukuvi.

Awali, Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria wa TLS, John Seka alisema wananchi wengi wamekuwa wakitumia mashamba kama rehani katika taasisi za fedha.

Alisema wamewasilisha juzi maoni yao kuhusu muswada huo katika Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria inayouchambua muswada huo.

Hata hivyo, alisema kwamba muswada huo unamtaka mmiliki wa mashamba ambayo hayajaendelezwa au yameendelezwa kidogo kutumia fedha anayoipata kwa kuweka rehani eneo lake, kuliendeleza na si vinginevyo.