Lukuvi atoa kauli fedha za mipango ya matumizi ya ardhi

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi

Muktasari:

Wizara ya Ardhi yasema imeweka mikakati kuhakikisha ardhi yote ya Tanzania inapangwa, kupimwa na kumilikishwa kisheria.

Dodoma. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amezitaka halmashauri kutenga fedha za kutosha kila mwaka kwa ajili ya mipango ya matumizi ya ardhi.

Lukuvi amesema mipango itasaidia kupanga na kupima kila kipande cha ardhi nchini kwa wakati.

Amesema wizara imeweka mikakati kuhakikisha ardhi yote ya Tanzania inapangwa, kupimwa na kumilikishwa kisheria.

“Mikakati inahusisha kuandaa programu ya kupanga, kupima na kumilikishwa kila kipande cha ardhi nchini,” amesema Lukuvi leo Aprili 20, 2018.

Waziri Lukuvi alikuwa akijibu swali la mbunge wa Karatu, Willy Qambalo aliyetaka kujua mkakati wa Serikali katika kuhakikisha ardhi yote ya Tanzania inapangwa na kupimwa kisheria ili kuondoa migogoro.

Lukuvi amesema Serikali inatambua umuhimu wa kupanga mipango ya matumizi bora ya ardhi nchini kama namna mojawapo ya kupunguza migogoro ya watumiaji na hasa wakulima na wafugaji