Waziri Makamba awataka Waislamu nchini kudumisha umoja

Muktasari:

Miaka mitatu imetimia tangu Mufti, Sheikh Abubakary Zubeir alipochaguliwa

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba amewata Waislamu nchini kudumisha umoja miongoni mwao na umoja wa kitaifa.

Makamba alitoa wito huo jana wakati wa hafla ya kumpongeza Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir akimwakilisha Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Hafla hiyo iliyoandaliwa na Jumuiya ya Vijana wa Kiislamu (Juvikiba) wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), ililenga kumpongeza Mufti Zubeir kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi cha miaka mitatu tangu alipochaguliwa.

Makamba aliwataka Waislamu kudumisha amani kwa kufuata misingi ya dini yao ambayo inasisitiza waishi kwa amani na umoja.

"Dumisheni umoja ndani ya uislamu, ndani ya Bakwata na umoja wa Kitaifa. Mambo hayo yalikuwa changamoto huko nyuma lakini Mufti amerudisha heshima ya uislamu nchini," alisema Makamba.

Waziri huyo alimpongeza Mufti kwa kazi anayoifanya ya kujenga Bakwata mpya na kuimarisha umoja miongoni mwa Waislamu na Watanzania kwa ujumla.

"Katika uongozi wake, Bakwata imepata uhai mpya, imepata marafiki wapya na inaonekana kuwakilisha Waislamu wote nchini. Mufti ameupa heshima uislamu, wakati mwingine jumuiya inadharauliwa kutokana na aina ya kiongozi wake," alisema.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mufti Zubeir alishukuru kwa pongezi hizo na kusema zimemwongezea hamasa ya kufanya kazi kwa moyo wote.

"Kupongezwa huku si sifa, sitachukulia kama sifa bali ni chachu ya kuuendeleza uislamu wetu na Taifa kwa ujumla," alisema.

Awali, akisoma risala ya jumuiya ya vijana hao, Katibu wa jumuiya hiyo, Athuman Zubery alitaja sababu za kumpongeza Mufti ni pamoja na kuwafanya Waislamu kuwa kitu kimoja.

Sababu nyingine, alisema Mufti ameanzisha ushirikiano na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi, amebuni vyanzo mbalimbali vya mapato, ameboresha maendeleo ya kitaaluma kwa Waislamu na ameanzisha ujenzi wa miundombinu ya Bakwata ikiwamo msikiti mkubwa Afrika unaofadhiliwa na Mfalme Mohamed VI wa Morocco.