Waziri Mkuu awapa tahadhari watumishi wa Umma

Muktasari:

  • Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana (Jumatatu, Februari 26, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya za Masasi na Nanyumbu kwa nyakati tofauti.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma wawatumikie wananchi kwa weledi na ustadi bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana (Jumatatu, Februari 26, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya za Masasi na Nanyumbu kwa nyakati tofauti.

Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Mtwara kwa ziara ya kikazi aliwasisitiza watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Amesema Rais Dk John Magufuli anataka watumishi wa umma wawatumikie wananchi bila ya ubaguzi wowote pamoja na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.

“Watumishi wa umma lazima mtambue kwamba msimamo wa Serikali ni kuwahudumia wananchi bila ya ubaguzi wa kidini, kiitikadi na kipato,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu amesema ni vyema watumishi hao wakaanza kujitathmini kwa sababu Serikali haitawavumilia watakaoshindwa kuwajibika kwa wananchi.

Pia amewataka watendaji hao kuacha urasimu na wahakikishe kila fedha iliyotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inatumika kama ilivyoelekezwa.

Waziri Mkuu amewaagiza watendaji hao wawe na mpango wa kuwatembelea wananchi kwa ajili ya kusikiliza kero zinazowakabili na kuzipatia ufumbuzi