Waziri Mkuu azindua kongamano la uwekezaji

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa 

Muktasari:

Katika kongamano hilo Waziri Mkuu amesisitiza juu ya vijana kujiajiri


Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua kongamano la tatu la Taifa la Uwekezaji na Uwezeshaji wa wananchi kiuchumi (NEEC) kuanzia ngazi ya mjini hadi vijijini.

Katika uzinduzi huo uliofanyika leo Jumatatu Juni 18, 2018 mjini Dodoma, Majaliwa amesema sekta zote zina jukumu la kuhakikisha zinatoa mchango kwenye uchumi wa viwanda.

Amesisitiza kuwa uwezeshaji huo kwa wananchi uende sambamba na kuwawezesha vijana kujiajiri.

“Kongamano hili la tatu linapaswa kuwa ni hatua muhimu ya kutathmini hatua mbalimbali tulizozifikia tangu tulipomaliza kongamano la pili lililofanyika mwaka jana,”amesema.

Amesema suala la uchumi wa viwanda ifikapo 2025 ni moja ya ajenda ya serikali ya awamu ya tano inayolenga kuwawezesha wananchi katika maeneo yenye fursa ikiwemo kutoa mikopo nafuu.