Waziri Mkuu kuhamaia Dodoma Septemba

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Muktasari:

Asema akishahamia, mawaziri na naibu mawaziri wote wafuatie mara moja

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema atahamia Dodoma ifikapo Septemba, mwaka huu kuonyesha kuwa Serikali imedhamiria kutekeleza ahadi ilizotoa kwa wananchi.

Ametoa kauli hiyo leo asubuhi wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa Dodoma na kuwashukuru kwa ushiriki wao kwenye maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa zilizofanyika kwa mara ya kwanza kwenye uwanja wa Mashujaa, mjini Dodoma.

“Jana nilimwita Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na kumwambia akamilishe matengenezo kwenye nyumba yangu kwa sababu ninataka kuhamia Dodoma ifikapo Septemba,” amesema Majaliwa na kushangiliwa na mamia ya wakazi wa mji wa Dodoma waliohudhuria maadhimisho hayo.

Amesema tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, kazi nyingi zimefanyika na wananchi wameziona na kwamba sasa hivi kazi iliyobakia ni utekelezaji wa ahadi alizotoa Rais John Magufuli.

“Wananchi kazi mmeziona na sasa tunaenda kwenye utekelezaji. Ninatoa agizo kuwa mawaziri na manaibu wote wahame mara moja kutoka Dar es Salaam na kuja Dodoma. Wana ofisi ndogo Dodoma na kwa kuwa wamekuwa wakiishi wakati wote wa Bunge, wahamie mara moja. Mimi nahamia Septemba na utekelezaji wake nitausimamia kwa juhudi zote,” alisisitiza.

Amewataka wakazi wa Dodoma watumie fursa hiyo kutunza amani ya nchi na kudumisha umoja uliopo na pia akataka watumie fursa hiyo kujenga nyumba za kuishi za kutosha, nyumba za kulala wageni na hoteli za kitalii ili watu watumishi na wageni wanapokuja wasipate taabu mahali pa kuishi.