Waziri Mkuu wa New Zealand atangaza kupata ujauzito

Muktasari:

 

  • Arden, ambaye ambaye alichaguliwa Oktoba mwaka jana kuwa Waziri Mkuu, amesema atajifungua mwezi Juni

Jacinda Ardern, ambaye aliapishwa kuwa waziri mkuu wa New Zealand Oktoba mwaka jana, alishangaza waandishi waliomuuliza kama alikuwa na mpango wa kuzaa kama angechaguliwa, alipowajibu kuwa "haikubaliki" kwa mwanamke kuwa na jibu la swali kama hilo akiwa kazini.

Lakini jana,  Ardern alitangaza kuwa anatarajia kujifungua mtoto wake wa kwanza mwezi juni. Alisema mwenzi wake, Clarke Gayford, mtangazaji wa televisheni wa kipindi cha uvuvi, atachukua likizo baada ya yeye kujifungua na kuwa mzazi wa kubakia nyumbani, gazeti la New York Times limeripoti.

Ingawa atakuwa kiongozi wa kwanza wa New Zealand kujifungua akiwa kazini, Ardern hakuchukulia kwa uzito wazo kwamba suala lake ni la kipekee, akisema yeye si "mwanamke wa kwanza kuwa na majukumu mengi" wala "kufanya kazi na kuwa na mtoto".

Lakini alikubali kuwa hali ya familia yake si ya kawaida kwa namna fulani, akisema amekuwa hajisikii vizuri nyakati za asubuhi za miezi mitatu ya mwanzo wakati akiunda serikali, na kwamba hajui ni kwa kwa vipi "magari ya serikali yatajisikia kuhusu kuwa na kiti cha mtoto".

Waziri mkuu huyo amesema amepanga kufanya kazi hadi atakapojifungua na baadaye atachukua likizo ya uzazi ya wiki sita. Katika kipindi hicho, alisema, naibu wake, Winston Peters, atakaimu.