Waziri Muhongo: Tumieni fursa zilizopo migodini kukuza uchumi

Muktasari:

Muhongo amewataka wananchi hao waunde vikundi vitakavyosaidia kupata mikopo hiyo itakayo wawezesha kuboresha mazingira yao ya uchimbaji.

Musoma. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewataka wakazi wa Musoma Vijijini mkoani Mara, kuacha kulalamikia hali ya umasikini walionao badala yake watumie fursa za migodi ya Kataryo na Etaro kukuza uchumi wao.

Waziri Muhongo ambaye pia ni mbunge wa Musoma Vijijini  amesema  kuwa wananchi wanatakiwa kuweka uhusiano mzuri na wawekezaji ili wasaidianae kutekeleza miradi ya maendeleo. “Kuweni na uhusiano mzuri kati yenu na wawekezaji wa migodi hii miwili ili kuinua miradi ya shule, barabara na afya badala ya kujenga uadui unaosababisha mkose fursa za kiuchumi,” amesema Profesa Muhongo. Amesema kuna Sh6.45 bilioni zimetengwa kwa ajili ya vikundi vya wachimbaji wadogo.

Amewataka wananchi hao waunde vikundi vitakavyosaidia kupata mikopo hiyo itakayo wawezesha kuboresha mazingira yao ya uchimbaji.

Diwani wa Kata ya Suguti, Denis Ekwabi amesema uwapo wa migodi hiyo katika halmashauri hiyo utasaidia kuongeza mapato pamoja na wananchi waliopo maeneo husika watanufaika kwa kupata ajira. Alisema wamejipanga kuhamasisha vikundi vya wanawake wajasiriamali wa kilimo ili waweze kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu wapate zabuni za kupeleka katika migodi hiyo. Amesema wameanza kuhamasisha jamii jinsi ya kujenga uhusiano mzuri na wamiliki wa migodi ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara.

Kiongozi wa kikundi cha ngoma cha Kariba, Boaz Songorwa alisema wananchi hawatarajii kuibuka tena migogoro badala ya kuwanufaisha.