Waziri Mwijage atoa masharti ya mikopo kwa wajasiriamali

Muktasari:

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amefungua maonyesho ya wanawake wajasiriamali Tanzania yaliyoandaliwa na Taasisi ya Tamasha la Mwanamke Mjasiriamali (Mowe) na kutoa agizo kuwa mjasiriamali asiyelipa kodi asipewe mikopo.


Dodoma. Wizara wa Viwanda, Biashara na Uwezekaji, Charles Mwijage amesema atashughulika na ofisa yeyote atakayempa mkopo mjasiriamali ambaye hajasajiliwa kama mlipa kodi.

Akizungumza leo Alhamisi Oktoba 18, 2018 katika Tamasha la Mwanamke Mjasiriamali, Mwijage ameagiza asipewe mtu yeyote fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Wajasiriamali Nchini (NEDF).

“Kama huna TIN number ambayo ni kuu kuu atakayekupa mkopo nitashughulika naye. Yaani ukija kuomba mkopo lazima uwe umejisajili TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) zaidi ya miezi mitatu iliyopita,” amesema.

Mwijage amesema anayetaka Serikali imbebe basi anapaswa na yeye kuibeba kwa kuchangia kidogo Serikali.

Pia, akawataka wajasiriamali hao kuhakikisha wanazalisha kwa wingi na wanapata nembo za ubora wa bidhaa zinazotolewa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) ambazo hutolewa bure katika miaka mitatu ya mwanzo.

Amesema iwapo Watanzania milioni 25 wenye uwezo wa kufanya kazi wangeweza kuchangia Sh15,000 kila mmoja mbali na kodi nyingine, Taifa lingeweza kupata fedha nyingi ambazo zingetumika katika miradi ya maendeleo.

“Naagiza asipewe mtu yeyote pesa ya NEDF ama pesa yoyote na nitatengeneza fitina hata kwenye ule mfuko wa Rais wasipewe, utaratibu wewe toa na wewe upewe,” amesema.

Amesema yajayo yanafurahisha kwa sababu mikopo watapewa wajasiriamali ambao wanalipa kodi na kwamba hali hiyo inafanana na watoa sadaka kwa Mungu.

“Mtu anakwenda kanisani anatoa Sh500 anamuomba Mungu ashinde mitihani yake halafu anashinda mtihani. Hivi kweli kushinda mtihani ni Sh500? Hata karo ya mwezi mmoja haitoshi,” amesema.

Mwenyekiti wa Tamasha la Mwanamke Mjasiriamali (Mowe) Zubeda Hiluwa amesema tamasha hilo limewasaidia wajasiriamali kuuza na kubadilishana uzoefu katika nchi za Afrika Mashariki bila woga wowote.