Waziri SMZ alalamika sukari ya Zanzibar kuzuiwa kuuzwa Bara

Meneja Mkuu wa kiwanda cha Sukari cha Zanzibar (ZSFL), Rajesh Kumar akionyesha mtambo wa kufua umeme kutokana na mabaki ya miwa (molasses) katika kiwanda hicho kilichopo Mahonda, Mkoa wa Kaskazini Zanzibar. Picha na Elias Msuya.

Muktasari:

Hata hivyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage alipoulizwa kuhusu malalamiko hayo alisema hana taarifa hadi awaulize wasaidizi wake.

Zanzibar/ Dar. Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko wa Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali amelalamikia katazo la Serikali ya Muungano kuzuia sukari inayozalishwa Zanzibar kuuzwa Bara akisema ni kinyume na matakwa ya Muungano na matakwa ya soko.

Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake mjini Zanzibar hivi karibuni, Balozi Amina alisema wamekuwa na majadiliano na Serikali ya Muungano kuhusu kadhia hiyo ambayo pia yataendelea mwisho wa mwezi huu.

Hata hivyo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage alipoulizwa kuhusu malalamiko hayo alisema hana taarifa hadi awaulize wasaidizi wake.

“Mimi ni waziri wa Viwanda na Biashara, nina manaibu waziri wawili, makatibu wakuu, manaibu katibu na nina wakurugenzi na mashirika 19 chini yangu. Ninasikia mambo mengi, nikikwambia nina majibu vidoleni nitakudanganya, hadi niwasikilize wasaidizi wangu,” alisema Mwijage kwa njia ya simu.

Akizungumzia kadhia hiyo, Balozi Amina alisema licha ya ukweli kwamba sukari inayozalishwa na kiwanda pekee cha Zanzibar Sugar Factory Ltd haitoshelezi mahitaji ya Wazanzibari bado wana haki ya kuuza popote wanapotaka.

“Mimi kama waziri wa Biashara na Viwanda niliona tuwe na ‘combination’ (muunganiko) kwamba sehemu wauze Zanzibar na nyingine wauze Bara, lakini Serikali ya Muungano haitaki kununua sukari kutoka Zanzibar. Sasa hilo nilitaka tuzungumze, kwa sababu siyo fair (haki),” alisema Balozi Amina na kuongeza:

“Arguments’ (hoja) kwamba haitoshelezi soko la Zanzibar si sahihi. Kwa sababu kama kiwanda kipo na kinazalisha, wana right (haki) ya kuuza Zanzibar au wakauza Bara. Kwa sababu kama ni hivyo kuna viwanda vya Bara vinauza Zanzibar lakini havijatosheleza soko la Bara, kwa sababu hili soko liko ‘free’ (huru) mtu anatakiwa ku ‘access’ soko kama anavyoona ni sawa.”

Waziri Amina aliyewahi kuwa Balozi wa Umoja wa Afrika nchini Marekani alisema madai kuwa Zanzibar haina kiwanda cha sukari na kwamba sukari hiyo inaagizwa kutoka nje ya nchi hayana msingi kwa kuwa kiwanda kipo na kimeshatembelewa na viongozi wakiwemo wa Serikali ya Muungano.

“Kwa hiyo wanapotuambia haiwezi kuuzwa Bara kwa sababu haitoshelezi Zanzibar, ‘that’s not right’ (siyo haki). Kwa sababu ‘fundamentally’ (kimsingi) huko ni kwenda kinyume na misingi ya soko na misingi ya huu Muungano wetu,” alisema.

“Sisi kama Serikali tunauza sukari ya Mahonda (ZSFL), mimi nilitoa kibali. Kipindi kile mgogoro wa sukari ulipoanza tulitoa barua rasmi nilimwandikia barua mpaka Waziri Mkuu nikimwambia sukari tunayowauzia ni ya Mahonda ambayo imekuwa certified (imethibitishwa) na ZBS na TBS na vyote.

“Wamekuja hadi watu wa Sugar Board (Bodi ya Sukari) wameona. Wanasema sukari yenu kidogo haitoshi Zanzibar, that’s not right, hiyo si sawa sawa, wapewe ‘access’ wauze, kama wanataka Bara wauze. Inakuwaje uruhusu sukari kutoka nchi za Sadc iingie Bara kwa nini wasiruhusu sukari ya Zanzibar iingie Bara?” aliendelea kuhoji.

Akizungumzia mahitaji ya sukari visiwani Zanzibar, Balozi Amina alisema kwa mwaka mzima hutumia kati ya tani 17,000 mpaka 20,000 za sukari huku kiwanda cha ZSFL kikizalisha zaidi ya tani 8,000.

Alisema kuna wafanyabiashara wanaoingiza sukari kutoka nje ya nchi ili kuziba pengo linalobaki ambao hata hivyo wamegoma kununua sukari ya kiwanda hicho wakidai ni bei ghali.

“Zanzibar maisha yako chini ndiyo maana Serikali iliamua ku ‘subsidize’ sukari, mchele na unga wa ngano. Hata hivyo wafanyabiashara wanaleta sukari inayofurika kwenye soko. Tukawaambia hao waagizaji kwanza wanunue sukari yote ya Mahonda, lakini ikaonekana kuwa wanauza sukari yao bei ghali kulinganisha na inayoagizwa,” alisema Balozi Amina.

Mwandishi wa gazeti hili alifika katika kiwanda cha ZSFL kilichopo Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja ambako Meneja mkuu, Rajesh Kumar alisema licha ya kuzalisha sukari kwa gharama kubwa wanapata hasara kwa kulikosa soko la Bara.

“Tunahitaji kuuza sukari yetu Bara ambako ni Sh95,000 hadi Sh100,000 kwa mfuko wa kilo 50, lakini hapa ni Sh60,000 hadi Sh70,000. Tumekuwa tukijadiliana na waziri wa biashara ili kutusaidia kupata soko la Bara. Tunajiuliza kama hii ni Tanzania moja na hata baadhi ya vifaa tunavyotumia kama mifuko ya sukari inatoka Dar es Salaam, lakini haturuhusiwi kuuza sukari tu Bara,” alisema Kumar.

Alisema kiwanda hicho kimeajiri rasmi watu 235 mbali na ajira zisizo rasmi na kina mitambo ya kisasa hivyo wanahitaji masoko ya uhakika hasa Bara.

“Kwa hiyo ni lazima tuuze sukari ili kiwanda kiendelee. Hiki ni kiwanda pekee na kikubwa Zanzibar cha sukari, tumeajiri wafanyakazi zaidi ya 235 hivyo tunahitaji msaada wa Serikali ili tuendelee,” alisema.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT), Miraji Kipande alisema hana taarifa ya katazo la sukari ya Zanzibar kuingia Bara, huku akisema kuna taratibu za kufuata ikiwa pamoja na kukata leseni.

“Kwa mujibu wa sheria ya Sukari ya mwaka 2001 na kanuni zake za mwaka 2010, zinaelekeza kuwa kampuni yoyote au mtu yeyote anayetaka kuingiza sukari nchini (Tanzania Bara) ni sharti apate leseni ya kuingiza bidhaa hiyo,” alisema Kipande.

Alisema bidhaa hiyo huingizwa baada ya kuidhinishwa na Serikali katika kipindi maalumu cha upungufu wa sukari nchini ambapo viwanda vya ndani vinasitisha uzalishaji kwa ajili ya matengenezo ya mitambo yao.

“Hata hivyo, Bodi ya Sukari haina taarifa kuhusu zuio hilo la sukari kwa kuwa mwaka 2016 kampuni hiyo iliruhusiwa na Serikali kuingiza sukari yao Bara,” alisema.

Kipande alikiri kuwepo kwa upungufu wa sukari akisema hadi Desemba 5, 2017 jumla ya tani 209,782.26 wakati lengo ni kuzalisha tani 308,558 kwa mwaka 2017/18.

Alisema bei ya sukari hupatikana kwa nguvu ya soko ambapo kwa sasa inauzwa kati ya Sh2,500 hadi 2,800 kwa kilo.