Waziri Tizeba aagiza kuwekwa bei elekezi pembejeo za kilimo

Waziri wa Kilimo, Charles Tizeba.

Muktasari:

Lengo ni kuzuia ulanguzi unaosababisha wananchi kushindwa kununua kutokana na bei kubwa.

Arusha. Waziri wa Kilimo, Charles Tizeba amewaagiza wadau wa pembejeo nchini kuweka bei elekezi za mbegu katika vifungashio ili kuwalinda wakulima wasilanguliwe.

Tizeba alitoa agizo hilo leo wakati akifungua mkutano wa wadau wa mbegu wenye lengo la kupashana taarifa kuhusu maendeleo ya sekta hiyo nchini.

Alisema ni lazima vifungashio vyote vya mbegu viwekwe bei elekezi ili kuzuia watu wanaofanya ulanguzi na kusababisha wananchi kushindwa kununua kutokana na bei kubwa kuliko uhalisia.

"Naombeni sana kila kifungashio kitakachokuwa kimebeba mbegu kiwe na bei elekezi na naagiza kuundwa kwa kamati ya pamoja ya kufuatilia mfumo wa uzalishaji na hizo bei elekezi, " alisema.

Tizeba pia alizitaka kampuni za mbegu zinazozalisha mbegu nje ya nchi na kuuza nchini kuzalisha mbegu hizo nchini ili kuongeza ajira kwa Watanzania na kulipa kodi na tozo mbalimbali.

Alisema iwapo kampuni zitazalisha mbegu hapa nchin zitapatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Patrick Ngwediagi aliwataka wafanyabiashara kupunguza uingizaji wa mbegu toka nje na badala yake  wazalishe hapa nchini.