Waziri Ummy akemea ndugu wa mgonjwa kutoa damu

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Muktasari:

Amesema kuwa huduma ya damu kwa mgonjwa yoyote yule anayehitaji kuongezewa damu ni bure na hakuna kutozwa gharama yoyote.

Dodoma. Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amepiga marufuku vitendo vya ndugu wa mgonjwa kutolewa damu ili mgonjwa wao apatiwe huduma ya kuongezewa damu.

 

Amesema kuwa huduma ya damu kwa mgonjwa yoyote yule anayehitaji kuongezewa damu ni bure na hakuna kutozwa gharama yoyote.

 

Waziri Mwalimu ametoa kauli hiyo jana jijini Dodoma kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya kuchangia damu duniani yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Mwalimu Nyerere.

 

Amesema wananchi wanachangia damu bure lakini wanakatishwa tamaa na watoa huduma za afya kwa kuwa ndugu zao wakiwa wanahitaji damu hulazimika tena kuchangia ili wahudumiwe.

 

"Ni marufuku mgonjwa kuuziwa damu tusitoe masharti ya ndugu wa mgonjwa kutozwa damu ndipo mgonjwa wao aongezewe damu, hii damu watu wanatoa bure itoeni bure sitaki kusikia tena huu utamaduni wa kuwatoza watu damu ili ndugu zao waongezewe," amesema Mwalimu.

 

Amewaagiza waganga wakuu wa Wilaya na Mikoa kuhakikisha kuwa mikoa yao inakuwa na damu salama ya kutosha kwa kuhamasisha watu kuchangia damu kwa hiyari.

 

Aidha aliwatoa hofu wananchi wanaoogopa kuchangia damu kwa kuogopa kupimwa Ukimwi na kusema kuwa kipimo cha VVU ni cha mwisho kabisa baada ya mtu kukamilisha zoezi la kutoa damu yake.

 

Kwa upande wake Mratibu wa Mpango wa damu salama Taifa Dk, Magdalena Lyimo alisema kwa muda wa siku nne za uhamasishaji wa kuchangia damu salama mkoa wa Dodoma umeweza kukusanya jumla ya chupa za damu 2,257.