Sunday, January 21, 2018

Waziri aagiza kigogo Wizara ya Maji asimamishwe kazi

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi eedward@mwananchi.co.tz

 Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe amemwagiza katibu mkuu wa wizara hiyo, Profesa, Kitila Mkumbo kumsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maji Mijini, Clement Kivegalo.

Mhandisi Kamwelwe amechukua hatua hiyo baada ya kutoridhishwa na utendaji wa mamlaka za maji za miji ambazo ziko chini ya idara inayoongozwa na Mhandisi Kivegalo.

Uamuzi wa kumsimamisha mkurugenzi huyo umekuja ikiwa ni mwendelezo wa hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kuvunja bodi za maji za mamlaka ya miji mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri Kamwelwe alisema haridhishwi na baadhi ya watendaji wa mamlaka za maji za miji na wizarani kwake na kusisitiza kuwa hatowavumilia.

“Juzi tu niliuondoa uongozi wa Mamlaka ya Maji ya Lindi kwa sababu kuna tatizo la utendaji wa makandarasi, hapa Dar es Salaam na Chalinze tuna tatizo, mamlaka za maji za miji ya mikoa zinasimamiwa na mkurugenzi wa maji mijini, hapa tuna idara kama tatu au nne zinasimamia utekelezaji wa miradi hiyo. Idara ya maji mijini inaongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mhandisi Clement Kivegalo wakati haya yote yanatokea yupo lakini matatizo yanabainiwa na waziri, naibu waziri au katibu mkuu,” alisema Waziri Kamwelwe.

Alifafanua kuwa juzi alizivunja bodi za maji safi za mkoani Arusha na Musoma mkoani Mara baada ya kujiridhisha kuwa utendaji wao si mzuri.

Sanjari na hilo waziri huyo pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma, Gantala Said na nafasi yake kuchukuliwa na Mhandisi Robert Lupoja wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza.

Mhandisi Kamwelwe pia alimuagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Mwanza (Mwauwasa) asaidie mamlaka ya Musoma ili waweze kufanya kazi inayotakiwa.

Utenguzi wa Said umekuja baada ya ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyofanya mkoani Mara na kubaini kasoro za utendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (Muwasa) na kuagiza hatua zichukuliwe ikiwamo kuchunguzwa watendaji wote.

-->