Waziri aeleza kwa nini kiwanda cha betri kilichelewa kupata kibali

Naibu waziri wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mussa Sima

Muktasari:

  • Wizara imetoa tamko hilo siku chache baada ya Rais John Magufuli kulaumu mamlaka husika kuwa zinakwamisha kiwanda hicho cha China Boda Technical Group Ltd kinachojengwa Kibaha mkoani Pwani kwa kutokipa kibali cha tathmini ya mazingira.

Kibaha. Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) imesema Tathmini ya Athari za Mazingira (EIA) haikuwa kikwazo kwa ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza betri, bali kunahitajika mabadiliko ya matumizi ya ardhi katika eneo kinapojengwa.

Wizara imetoa tamko hilo siku chache baada ya Rais John Magufuli kulaumu mamlaka husika kuwa zinakwamisha kiwanda hicho cha China Boda Technical Group Ltd kinachojengwa Kibaha mkoani Pwani kwa kutokipa kibali cha tathmini ya mazingira.

Lakini jana, naibu waziri wa wizara hiyo, Mussa Sima aliyeagizwa na Rais Magufuli kwenda kulishughulikia suala hilo siku akiapishwa, aliieleza Mwananchi kuwa wawekezaji hao wamekamilisha mchakato wa EIA na wamekabidhiwa cheti kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa kiwanda hicho.

Sima alisema katika mchakato wa EIA wa mradi huo kulikuwa na changamoto ya matumizi ya ardhi ya eneo hilo na aina ya uwekezaji unaofanyika.

“Baada ya kufika hapa nimejionea hali ilivyo na kwamba mwekezaji huyu hakupata cheti cha mazingira kwa wakati kutokana na eneo hili kuwa limetengwa kwa viwanda vidogo,” alisema.

Alisema kiwanda hicho ni kikubwa na kinahusisha kemikali hatarishi na kwamba mamlaka zilitakiwa kubadilisha matumizi ya ardhi ili waweze kukamilisha mchakato wa tathmini.

“Hata hivyo, pamoja na kupatiwa cheti cha EIA, wamiliki wa kiwanda hiki wanatakiwa kuzingatia masharti mahsusi yanayoambatana na cheti hiki ambapo pamoja na mambo mengine, mwekezaji anatakiwa kukamilisha kubadili matumizi ya ardhi kabla ya kuanza uzalishaji ili uwekezaji huu uendane na matumizi ya ardhi ya eneo hili,” alisema. Naibu waziri huyo alitoa maelekezo kwa mikoa baada ya kubaini uwepo wa changamoto ya matumizi ya ardhi ambayo inayakabili maeneo mengi yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji na kuchangia katika kuchelewesha mchakato wa tathmini ya athari za mazingira wa miradi ya ujenzi wa viwanda.

“Natoa wito kwa viongozi wa mikoa, wilaya, halmashauri na taasisi zote nchini kuhakikisha kwamba wanafanya Tathmini ya Mazingira Kimkakati (SEA) katika maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji katika maeneo yao,” alisema Sima.

Alisema hali hiyo itasaidia kurahisisha mchakato wa tathmini ya athari kwa mazingira.

Sima alisema taasisi kama Nemc, Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi zifanye kazi kwa karibu na ushirikiano ili kuondoa vikwazo.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Ndikilo alisema Nemc walishatekeleza wajibu wao wa kutoa cheti cha tathmini ya athari za mazingira na changamoto imebaki kwa NDC na Wizara ya Ardhi.

“Bado tuna changamoto na NDC kwa kuwa nyaraka zao hazionyeshi kuwa hili eneo ni kwa ajili ya viwanda vikubwa au la,” alisema Ndikilo.

Julai 2, Rais John Magufuli alisema Nemc imeshindwa kutoa kibali kwa kiwanda hicho na kutaka kitolewe vinginevyo atakitoa yeye.

“Vibali vya Nemc visiwe vinachelewa,” alisema.

“Kuna kampuni moja hapa Kibaha imekuja kuwekeza dola 1.5 milioni za Marekani. Wameshajenga zaidi ya asilimia 59 na vifaa vingine viko bandarini.

“Mpaka leo hamjawapa kibali na issue mnasema itaharibu environment (mazingira) wamekuja kuwekeza hapa kiwanda cha betri dry cell (zisizotumia maji). Watatengeneza ajira, Serikali itakusanya mapato. Nataka vibali vitoke mapema, kasimamieni hili.”

Alisema kuna baadhi ya vitengo Nemc vina watu wa ajabu na hivyo kutaka wasimamiwe.

“Otherwise (vinginevyo) hili suala la kuendeleza viwanda halitakuwepo kama wanakwamisha na watu wengine,” alisema Rais.

“Nilichofanya nilimweleza mkuu wa Mkoa wa Pwani wapangie (siku) nitakuja kuweka jiwe la msingi au kufungua. Nitatoa kibali cha Nemc siku hiyo, kwa hiyo subirini nitatoa kibali siku nikienda kuweka jiwe la msingi, kwa hiyo kashughulikieni hili.”