VIDEO:Waziri aomba radhi sakata la samaki bungeni

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhanga Mpina akizungumza bungeni leo alipokuwa akiomba  radhi Bunge na wabunge kwa kile kilichotokea jana kwa maofisa wa wizara yake kuingia bungeni na kukamata samaki waliovuliwa kimakosa. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Waziri huyu alikiri utekelezaji wa operesheni sangara ulikuwa na matatizo katika jambo hilo


Dodoma. Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameliomba radhi Bunge na wabunge kwa kile kilichotokea jana Juni 19, 2018 kwa maofisa wa wizara yake kuingia bungeni bila ridhaa.

Akitoa taarifa ya Serikali bungeni leo Juni 20 kuhusu kilichotokea jana, Mpina amesema sehemu ya utekelezaji wa shughuli za wizara ikiwamo operesheni sangara ambayo jana ilitendeka bungeni, itaendelea lakini kwa bahati mbaya utekelezaji huo haukuzingatia tararibu za Bunge.

Amesema Juni 19 akiwa katika mgawaha wa Bunge aliona samaki wa sato akahisi wapo chini ya sentimita 25.

“Nikamuagiza katibu wangu, kwamba wakaguzi wakajiridhishe na samaki hao na wakaguzi walimuhoji muuzaji mgahawa ambaye alikiri ni wachanga walikuwa chini ya sentimita 25,” amesema.

Ameongeza: “Napenda kukiri kwamba watumishi katika kutekeleza kazi hiyo waliingia bila kibali, kupima chakula kilichopikwa na kwa taratibu hizo, wizara inaliomba radhi Bunge lako tukufu na wewe mwenyewe.”

Mara baada ya kauli hiyo, Spika Job Ndugai amesema anamshukuru Mpina kwa maelezo yake lakini akaongeza kuwa, kilichofanywa na maofisa hao ni dharau ya juu.

“Tumshukuru waziri kwa maelezo aliyoyatoa, lakini kwa waziri mkuu tunasikitishwa sana na kilichotokea, sisi si Bunge pekee duniani, sisi ni jumuiya ya kimataifa, wenzetu wakisikia kuna waziri na maofisa walichofanya ni dharau ya juu sana,”amesema.

Amesema linapotokea kosa la jinai katika eneo la Bunge, kamanda wa polisi ana wajibu wa kumjuluisha Spika kwani Bunge halilindi Spika.

 “Wapimaji wa wizara wanapima samaki mikono haina hata gloves, mikono wazi, wanashika shika, si wao peke yao, wamealika na waandishi wa habari, yaani ni kama mpango fulani wa kuliweka Bunge kusipostahili, kwa hiyo aaaaaaaa, kwa kawaida naomba tukubaliane nami, ukiwa umekasirika sana unapaswa kusamehe,”amesema.

Hata hivyo, baada ya kauli hiyo Bunge lilikaa kimya ghafla na wabunge kadhaa wa CCM na upinzani wakasimama kuomba mwongozo lakini hawakupewa fursa hiyo.