Waziri apokea mabilioni ya Ukimwi akitaja mbinu mpya ya wanaojiuza

Naibu waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile

Muktasari:

  • Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa miaka mitatu uitwao Amref Health Afrika wa kupambana na maambukizi mapya ya Ukimwi na kifua kikuu unaofadhiliwa na GF, naibu waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema jana kuwa utekelezaji wake unahitaji ubunifu na kwenda na wakati.

Dar es Salaam. Wakati watu wanaouza miili wakibadili mbinu na kuhamia mitandaoni tofauti na awali walivyozoweleka kujipanga barabarani usiku, Serikali imepokea Sh55 bilioni kutoka Global Fund (GF) ili kukabiliana na maambukizi mapya ya Ukimwi na kifua kikuu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa miaka mitatu uitwao Amref Health Afrika wa kupambana na maambukizi mapya ya Ukimwi na kifua kikuu unaofadhiliwa na GF, naibu waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema jana kuwa utekelezaji wake unahitaji ubunifu na kwenda na wakati.

“Kwa mfano zamani wanaouza miili yao walikuwa wanajipanga barabarani na kwenye madanguro, lakini sasa wanatumia mtandao na nyinyi mnapaswa mjipange na kujua mtawafikia vipi huko walipo, fedha hizi ni nyingi zinahitaji umakini wa hali ya juu,” alisema Dk Ndugulile.

Alisema ili kuwafikia walengwa wa mradi huo wahusika hawana budi kuwa wabunifu kwa kwenda na wakati unaotumia teknolojia.

Dk Ndugulile alisema Serikali itashirikiana na wale watakaokuwa wakitekeleza mradi huo kwa kila njia na milango ipo wazi kwa ajili ya ushauri na utatuzi wa changamoto.

“Sitaki visingizio, eti baada ya miaka miwili ya utekelezaji ndio mnakuja na kauli kuwa hamkufanikiwa kwa sababu ya changamoto fulani, sitawaelewa zisemeni mapema zifanyiwe kazi kwa matokeo chanya,” alisema.

Naibu waziri alisema Amref wamekabidhiwa jukumu hilo kama dhamana ili washirikiane na asasi nyingine. “Hakikisheni mnawasimamia ipasavyo mnaokwenda kufanya nao kazi kwa sababu fedha hizo ni za Watanzania na zinapaswa kutumiwa kwa manufaa yao,” alisema.

Kuhusu changamoto ya wanaume kutojitokeza kwa wingi kupima afya zao na kuchelewa kutumia dawa za kufubaza maambukizi ya Ukimwi, Dk Ndugulile alisema fedha hizo zitumike kuwafikia.

“Nasisitiza fedha hizi zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya kutumika bila kufikia malengo au kutumika kidogo kutokana na kutokuwa na mikakati madhubuti,” alisisitiza.

Mkurugenzi mkazi wa Amref, Dk Florence Temu alisema mradi huo unalenga kupunguza maambukizi mapya ya kifua kikuu kwa asilimia 20 na vifo vitokanavyo na Ukimwi kwa asilimia 35 kulingana na takwimu zilizopo.

Alisema mradi ulianza kutekelezwa mwaka huu na unatarajiwa kukamilika 2020, huku unakikusudia kuwafikia watu 546,880 watakaopatiwa huduma ya upimaji wa virusi vya Ukimwi (VVU) na kuwapa majibu yao.

Dk Temu alifafanua kuwa mradi huo pia utawapatia huduma hiyo wasichana waliovunja ungo na wanawake 162,064 pamoja na kuwapa rufaa watu 16,465 wenye maambukizi ya kifua kikuu.

Aliongeza kuwa mradi unatarajiwa kufika katika mikoa 15 ikiwamo Arusha, Dodoma, Kilimanjaro, Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara, Mwanza, Pwani, Shinyanga, Simiyu, Singida, Tanga na Ruvuma.

“Tunashirikiana na asasi nne ambazo kila mmoja atapewa majukumu yake katika kuhakikisha kila kilichopangwa kinafanyika ipasavyo,” alisema Dk Temu.

Alisema Amref inatambua changamoto ya kuwafikia wanaume kupima na watu wengi kutojua hali zao, ambapo takwimu za utafiti wa hali ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi (HIV impact survey) inaonyesha asilimia 52.2 ya walio na umri wa miaka 15 hadi 64 ndio waliopima na kujua hali zao.

“Tutahakikisha tunawafikia wanaume kwa wingi na kundi hatarishi la maambukizi ambalo ni vijana,” alisema Dk Temu.