Waziri wa Fedha afichua siri ya watu ‘kuchacha’

Muktasari:

  • Hivyo, amewataka wachumi kuhamasishana kutafuta nafasi za ubunge ili wasaidie wananchi na Taifa wakiwa bungeni.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema licha ya nchi kuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa Pato la Taifa, umekuwa hauonekani katika maisha ya watu walio wengi kutokana na kasi ndogo ya ukuaji wa sekta ya kilimo iliyo chini ya wastani wa asilimia tatu.

Hivyo, amewataka wachumi kuhamasishana kutafuta nafasi za ubunge ili wasaidie wananchi na Taifa wakiwa bungeni.

“Kule tulipo mimi na mheshimiwa Mwigulu, ikitokea Mwiguku katoka wachumi waliopo pale wanahesabika, lakini sehemu kama ile ya kutungia sheria halafu wachumi ni wachache mimi naona ni shida, lakini chombo hiki kinaweza kushawishi kupatikana kwa wachumi wengi ili kunyoosha mambo,” alisema Dk Mpango.

Alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Jumuiya ya Wachumi Tanzania (EST) katika ukumbi wa Benki Kuu (BoT) jijini Dar es Salaam akiwa mgeni rasmi.

Dk Mpango alisema anaamini kupitia jukwaa hilo wachumi watahamasishana kutafuta nafasi ya kuingia bungeni ili kusimamia mipango ya uchumi ya nchi.

Waziri Mpango alisema changamoto nyingine ya ukuaji wa pato ni ukosefu wa ajira kwa asilimia 10.3 na kiwango cha umaskini kwa asilimia 15, huku ongezeko la watu likiwa asilimia 2.7 kwa mwaka. “Sekta ya fedha imekumbwa na msukosuko wa kuongezeka kwa mikopo chechefu kwa asilimia 12.5 licha ya kiwango cha BoT kuwa ni asilimia tano; riba za kukopa kuwa juu; ongezeko dogo la kiwango cha mikopo na baadhi ya biashara kudorora hasa zile ambazo zilikuwa hazilipi kodi na zenye madeni makubwa,” alisema Dk Mpango.

Nyingine alisema ni wabia wengi wa maendeleo kutoka nje ya nchi kuchoka kutoa misaada ya kibajeti; kuongezeka gharama za mikopo katika benki na taasisi za kifedha za kimataifa na ulaghai unaotekelezwa na kampuni ya uwekezaji kupitia mikataba isiyo na tija kwa Taifa.

Dk mpango alisema ameeleza hayo ili kuwapa wachumi nafasi kupitia EST kufikiri namna watakavyokusanya nguvu na maarifa katika kuongeza kasi ya kuibadilisha Tanzania kuwa kitovu cha uchumi katika bara la Afrika kupitia weledi wao, bidii, uzalendo, uwazi na uwajibikaji.

“Ningependa kuona jumuiya ya wachumi ambayo inajinasibisha kwa umahiri wa kukuza tafiti za kiuchumi, maendeleo ya nchi, mafunzo kwa wachumi kazini, kuratibu jukwaa la mijadala kuhusu sera za kiuchumi, kuibua mawazo mbadala yanayotekelezeka kwa ajili ya kuiinua nchi na kuratibu mifumo ya mahusiano na wachumi wengine,” alisema Dk Mpango.

Awali, Gavana wa BoT, Profesa Florens Luoga alisema hatua ya kurejeshwa kwa jumuiya hiyo ambayo ilikuwa imekufa tangu mwaka 1999 imekuja wakati muafaka kwa kuwa nchi ilikosa jukwaa la kujadili na kuangalia mwelekeo wa uchumi na maendeleo, kutoa tahadhari au ushauri kwa wakati ili kusaidia pale mambo yanapokwenda sivyo.

“Chama cha wachumi ni nyenzo muhimu ya kukuza na kuhakikisha uhai wa wachumi kama ilivyo kwa taaluma nyingine kama vile wanasheria, wahandisi na wahasibu. Chama hiki kinapaswa kuhakikisha uadilifu na elimu endelevu kwa wanachama na hata kuimarisha mafunzo ya uchumi,” alisema Profesa Luoga.

Mwenyekiti wa kamati ya kufufua jumuiya hiyo Geoffrey Mwambe ambaye pia ni mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) aliwaomba wachumi kuiombea jumuiya hiyo iliyosajiliwa kama taasisi isiyo ya kiserikali idumu.

Alisema itakuwa na jukumu kubwa la kusimamia ustawi wa uchumi katika nchi.

“Tutakuwa na jukumu la kuwakilisha maoni ya wachumi, kujadili changamoto za sekta ya uchumi na kuzitafutia ufumbuzi kupitia utafiti, mijadala na uchambuzi wa sera. Tutakaa mbali na sababu zilizosababisha kifo cha jumuiya ile iliyoanzishwa mwaka 1966,” alisema Mwambe.