Waziri wa Fedha atajwa kukwamisha miradi ya maendeleo

Muktasari:

Yaelezwa akiendelea kuwa waziri, miradi mingi zaidi itakwama


Dodoma. Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali amesema  Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ni miongoni mwa mawaziri  waliofeli kwa kukwamisha miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali.

Bobali ametoa kauli hiyo leo Mei 24, 2018 katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati mwaka 2018/19.

Amesema miradi ya umeme vijijini na mingineyo inakwama kwa kuwa waziri huyo hatoi fedha licha ya Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani kuzindua miradi mbalimbali ya Wakala wa Umeme Vijijini (Rea).

“Kama Dk Mpango ataendelea kuwa waziri kwa miaka mitano  atakwamisha miradi mingi na kama kuna waziri aliyefeli zaidi ni Mpango. Wizara ya Kilimo, Maji, Tamisemi zimelia hazina fedha, “ amesema.

Bobali amemtaka Dk Kalemani atakapokuwa akihitimisha hoja yake kueleza utekelezaji wa mpango wa umeme wa Power Afrika uliozinduliwa mwaka 2013 na aliyekuwa Rais wa Marekani, Barack Obama.

“Waziri ukija utueleze Power Africa imefikia wapi kuna taarifa Power Africa iliondoka baada ya Rais Kikwete (Jakaya-rais wa Awamu ya Nne) kuondoka madarakani,” amesema.

Kwa upande wake mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara amesema wabunge wanamsubiri Dk Mpango atakapowasilisha bajeti yake bungeni  kutokana na wizara yake kushindwa kutoa fedha z amiradi ya maendeleo.

“Dk Mpango watu wanakusubiri utuambie kama fedha hakuna tupange namna ya kupata fedha. Ili watu watoke gizani na wasitumie mkaa ni lazima umeme na gesi uuzwe kwa bei nafuu. Ukonga tu pale hakuna umeme, mimi pale nina mitaa tisa  haina umeme, mingine miwili ya kata ya Msongola hakuna umeme, Chanika, Buyuni nako hakuna umeme,”amesema.