VIDEO: Waziri wa Maji atengua uteuzi wa Ofisa Mtendaji Mkuu Dawasa

Waziri wa Maji na Umwagialiaji, Mhandisi Isack Kamwelwe 

Muktasari:

  • Avunja bodi ya wakurugenzi Dawasa


Dar es Salaam.Waziri wa Maji na Umwagialiaji, Mhandisi Isack Kamwelwe ametengua uteuzi wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (Dawasa), Mhandisi Romanus Mwang'ingo kwa tuhuma za udanganyifu na ubadhirifu wa mradi wa kuchimba visima vya Kimbiji na Mpera, Manispaa ya Kigamboni.

Mbali na hilo, Mhandisi Kamwelwe kwa idhini ya Rais John Magufuli amevunja bodi ya wakurugenzi wa Dawasa kwa kushindwa kuchukua hatua mapema katika kunusuru mradi huo.

Waziri  huyo, ametangaza uamuzi huo leo Jumatatu    Juni 18, 2018 wakati akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam.

"Jambo hili, linachunguzwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na Serikali imefikia hatua hii ili kuweka mazingira mazuri ya uchunguzi,"amesema Mhandisi Kamwelwe

Hata hivyo, kwa mamlaka aliyokuwa nayo, Mhandisi Kamwelwe amemteua Dk Sufian Masasi kukaimu nafasi ya Mwang'ingo hadi utaratibu mwingine utakapokamilika.