Wazungu wamtembelea mtengenezaji helikopta Tunduma

Muktasari:

Kijana Kinyekile ambaye pia ni fundi magari alitumia ubunifu wake kuunda helikopta, kitu ambacho kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, George Mbijima akiwa mjini Tunduma alimtembelea kisha kuweka jiwe la msingi kwenye helikopta hiyo.

Mbeya. Mkazi wa Tunduma, mkoani  Songwe, Adam Kinyekile (34)  ambaye alikuwa akitengeneza helikopta amepata mwaliko maalumu na wazungu kutoka Afrika Kusini  kutembelea kiwanda chao cha kutengeneza chopa.

Kijana Kinyekile ambaye pia ni fundi magari alitumia ubunifu wake kuunda helikopta, kitu ambacho kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa, George Mbijima akiwa mjini Tunduma alimtembelea kisha kuweka jiwe la msingi kwenye helikopta hiyo.

Hata hivyo baada ya taarifa za kijana huyo kurushwa kwenye vyombo vya habari , Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ilipiga marufuku kwa mtu yoyote kutojihusisha na utengenezaji au ubunifu wa ndege bila kufuata taratibu.

 Onyo hilo lilionekana kumlenga Kinyekile kwa kazi yake aliyokuwa akiifanya jambo ambalo lilimfanya asiweze kuendelea na maboresho ya helikopta yake licha ya kudai ilikuwa imebaki kuruka.

Akizungumza jana, Kinyekile alisema Alhamisi ya wiki hii alitembelewa na wazungu waliodai ni Raia wa Afrika Kusini kutoka kiwanda cha kutengeneza helikopta na  kutaka kuonana naye ili wajionee kazi yake waliyoiona kwenye mitandao.