Wazungu wamwalika mtengeneza helkopta

Wananchi wakitazama helikopta iliyotengenezwa na Adam Kinyekile.

Muktasari:

Kinyekile ambaye pia ni fundi magari, alitumia ubunifu wake kuunda helikopta iliyomvutia Kiongozi wa Mbio za Mwenge, George Mbijima akiwa mjini Tunduma ambaye alimtembelea kisha kuweka jiwe la msingi kwenye helikopta hiyo.

Mbeya. Mkazi wa Tunduma mkoani  Songwe, Adam Kinyekile (34)  ambaye ametengeneza helikopta amepata mwaliko maalumu wa Wazungu kutoka Afrika Kusini, ili kutembelea kiwanda chao cha kutengeneza chopa.

Kinyekile ambaye pia ni fundi magari, alitumia ubunifu wake kuunda helikopta iliyomvutia Kiongozi wa Mbio za Mwenge, George Mbijima akiwa mjini Tunduma ambaye alimtembelea kisha kuweka jiwe la msingi kwenye helikopta hiyo.

Hata hivyo, baada ya taarifa za kijana huyo kurushwa kwenye vyombo vya habari, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ilipiga marufuku mtu yeyote kujihusisha na utengenezaji, au ubunifu wa ndege bila kufuata taratibu.

 Onyo hilo lilionekana kumlenga Kinyekile kwa kazi yake, jambo ambalo lilisababisha  asiendelea na maboresho ya helikopta yake licha ya kudai ilikuwa imebaki kurushwa.